Na WAF - DSM.
KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuweza kujua hali zao mapema na kuepuka dhidi ya magonjwa ikiwemo Saratani inayo pelekea kifo pindi mgonjwa anapochelewa kuanza matibabu.
Prof. Makubi ametoa wito huo leo wakati akiongea na Waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa Kongamano la 8 la Kisayansi la masuala ya tafiti na mafunzo lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili, Jijini DaresSalaam. Kauli mbiu ikiwa "utafiti na mafunzo ni daraja la kuelekea huduma bora kwa wagonjwa wa saratani ya damu."
"Nitoe wito kwa Wananchi kuwahi kufanya uchunguzi ili kujua hali ya magonjwa hasa ugonjwa wa Saratani katika miili, dalili za ugonjwa wa Saratani tunazijua, zipo nyingi, inawezakuwa kupungukiwa damu, inaweza kuwa kujisikia homa, inawezakuwa kupungua uzito au kukohoa damu kwa wagonjwa wenye kansa za Kifua, au hata kushindwa kula chakula." Amesema.
Aliendelea kusema kuwa, endapo mtu amepata dalili zozote kati ya hizi ni vizuri kwenda mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kufanya uchunguzi kujua hali ya afya na kuanza matibabu, kwani yaweza kuwa ni ugonjwa wa Saratani au ugonjwa mwingine, amesisitiza Prof. Makubi.
Sambamba na hilo, Prof. Makubi amesisitiza kuwa, ni vizuri kila baada ya miezi sita mpaka mwaka mmoja kujenga tabia ya kwenda kufanya uchunguzi (check up) ili kujua hali ya afya ya mwili, ikiwamo kuangalia magonjwa yasiyoambukiza kama vile ugonjwa wa Saratani.
Aidha, Prof Makubi amesema kuwa, takribani watu 40,000 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, huku akisisitiza kuwa asilimia 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha kwasababu ya kuchelewa kufanya uchunguzi ili kuanza matibabu ya ugonjwa wa Saratani.
"Takribani watu elfu 40 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa Tanzania, na 80% ya wagonjwa hawa hupoteza maisha."amesema Prof Makubi
Hata hivyo, Prof Makubi ameushukuru uongozi wa Chuo cha Muhimbili kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani.
Vile vile, Prof. Makubi amewashukuru Wataalamu mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika kusaidia tiba ya magonjwa ya Saratani ya damu, Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Magesa (Daktari wa Haematology, Chuo cha Muhimbili), Dkt. Maunda (Taasisi ya Saratani Ocean Road), Dkt. Trish (Daktari wa Watoto).
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Andrea Pembe amewashukuru Wataalamu na wanafunzi waliojitokeza kushiriki Kongamano hili la Kisayansi lenye kujadili Saratani ya Damu lenye lengo la kutafuta matibabu ili kuwasaidia wananchi wanaopoteza maisha kwasababu ya ugonjwa wa Saratani, hasa Saratani ya damu.
MWISHO.
Post A Comment: