Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameshuhudia utiaji Saini Mkataba wa Utafiti wa Gesi ya Heliam kati ya Kampuni ya Noble Helium Limited kupitia Kampuni yake Tanzu ya Rocket Tanzania Limited na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Utafiti wa Gesi ya Heliam katika maeneo mbalimbali nchini.
Utafiti huo, utahusisha maeneo manne tofauti ikiwemo eneo la Ziwa Nyasa, Ziwa Eyasi, Ziwa Rukwa pamoja na Ziwa Manyara ambapo mradi huo utaajiri wafanyakazi wake wote kutoka Tanzania na wafanyazi wasiozidi kumi watatoka nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kiruswa amesema viashiria vya uwepo wa gesi ya heliam katika maeneo mbalimbali ya nchi ni uthibitisho tosha unao onesha kubarikiwa kwa nchi ya Tanzania, kwani ni madini ambayo yanategemewa kuongeza Pato la Taifa kwa kuwa yanahitajika sana kwenye shughuli za uchumi wa kileo.
Pia, Dkt. Kiruswa ameishauri Kampuni ya Rocket Tanzania Limited kuishirikisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kuwa ina taarifa nyingi za awali za uwepo wa madini katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sababu shirika hilo linafanya shughuli za utafiti wa madini na lina vifaa vya kutosha vya utafiti.
"Naomba nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake mazuri anayotupa sisi wasaidizi wake, anataka kuona mazingira ya uwekezaji nchini yanakuwa bora na ya kuvutia," amesema Dkt. Kiruswa.
Imeelezwa kuwa, uhaba wa gesi hiyo kote duniani ulikuwa umesababisha taharuki hususan kwa madaktari ambao wanatumia gesi hiyo kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama MRI scanners, pia heliam hutumika katika teknolojia ya kutengeneza vifaa vya maabara, roketi, mitambo ya kinyuklia, vifaa vya elektroniki na vifaa vingine vingi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye amempongeza Naibu Waziri kwa kukubari kuja kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo ambapo amesema mradi hou utainufasha Tanzania kwa kuongeza pato la taifa na kuongeza ajira kwa watanzania.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba ameitaka Kampuni ya Rocket Tanzania Limited kuhakikisha inawasilisha taarifa za utafiti wanaoutanya kila baada ya miezi mitatu.
Wakati huo huo, Dkt. Budeba ameiahidi Kampuni hiyo kuipa ushirikiano wa kutosha katika shughuli zao ya utafiti wa gesi hiyo wanaoufanya katika maeneo mbalimbali pindi watakapo hitaji msaada kutoka GST.
Kwa upande wake, Meneja wa Ushiriki na Ushirikishwa wa Wazawa katika Uchumi wa Madini (Local Content) wa Tume ya Madini Jofrey Nsemwa ameitaka Kampuni ya Rocket Tanzania Limited kuhakikisha inawasilisha Mpango wa Ushiriki na Ushirikishwaji wa Wazawa katika Uchumi wa Madini ambao wameuandaa katika kutekeleza shughuli yao ya utafiti.
Ikiwa imepita miezi mitano (5) tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Kushuhudia utiaji Saini wa Mikataba minne (4) ya uchimbaji mkubwa wa madini hatimaye leo Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameshuhudia utiaji Saini wa Mkataba wa Utafiti wa Gesi ya Helium kati ya Kampuni ya Noble Helium Limited kupitia Kampuni yake Tanzu ya Rocket Tanzania Limited na Chuo Kiuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Utafiti wa Gesi ya Heliam katika maeneo mbalimbali nchini, hakika ni mafanikio makubwa.
Post A Comment: