Mwandishi wetu, Arumeru


Jumla ya kiasi cha milioni 540 zimetumika kugharamia ujenzi na vifaa vya kisasa katika jengo la upasuaji  wa watoto waliopinda miguu katika hospitali ya Nkoaranga wilayani Arumeru mkoani Arusha.


Fedha hizo zimetolewa kwa ufadhili wa serikali ya Ujerumani chini ya programu ya Aktion Feuerkinder inayotekelezwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka nchini Marekani.


Akizungumza na waandishi wa habari  Mkurugenzi wa hospitali ya Nkoaranga, Dkt. Samwel Kiwesa alisema kwamba zaidi ya watoto 2,000 wenye matatizo ya kupinda kwa miguu na vifundo wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji na kupona.


Dkt. Kiwesa alisema kwamba asilimia kubwa ya watoto wanaofika hospitalini hapo kupatiwa matibabu wanatoka katika mikoa ya Iringa,Mwanza,Manyara na Arusha.


Dkt. Kiwesa alisema kwamba jamii inapaswa kuondoa dhana ya kwamba mtoto anayezaliwa amepinda miguu ana laana au nuksi bali wanapaswa kuwapeleka hospitalini mapema kupata matibabu.


"Suala la ushirikina halipo hili ni suala la uumbaji wa Mungu tuondoe dhana kwamba mtoto aliyezaliwa amepinda miguu amerogwa hapana wapelekeni hospitali mapema" alisema Dk Kiwesa


Naye Dk Annemarie Schraml Ameeleza kuwa tatizo la matumizi ya maji yenye kemikali nyingi aina ya Fluoride linachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la watoto kupinda miguu.


Dkt Schraml ambaye ni bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka nchini Ujerumani alisema kwamba jamii haipaswi kuwaficha watoto waliopinda miguu majumbani bali wawafikishe hospitalini ili wapatiwe matibabu.


Hata hivyo,Grace Ayo ambaye ni muuguzi katika chumba cha upasuaji alisema kwamba wazazi wengi wanashindwa  kumudu matibabu kutokana na gharama kuwa nyingi.


Rehema Emmanuel ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji na kufanikiwa kupona katika hospitali hiyo alisema kwamba awali alionekana amezaa mtoto wa ajabu baada ya kuzaa mtoto aliyepinda miguu.


"Awali nilionekana nimezaa kitu cha ajabu wengi walinishangaa sana lakini baadhi yao walinitia moyo jamii isiwanyanyapae watoto waliopinda miguu na wasiwafungie ndani" alisema Rehama

Share To:

Post A Comment: