Moses Mashalla, Arusha 


Mstahiki Meya Jiji la Arusha, Maxmillian Matle Iranqhe amekemea tabia ya baadhi ya watu kuwanyanyapaa watoto na watu wenye ulemavu (usonji) na kuitaka jamii kujenga tabia ya kuwapenda kuwajali na  kuwathamini .


Pia ameshauri jamii  kuwapa fursa walemavu hao badala ya kuwanyanyapaa kwa kuwa hawakuchagua kuwa na hali hiyo Bali ni uumbaji wa Mungu.


Meya huyo  alitoa kauli hiyo   wakati wa  maadhimisho ya siku ya usonji duniani katika Jiji la Arusha ambapo alialikwa kama mgeni rasmi.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Meya Maximilian alisema kwamba walemavu wana haki ya kushirikishwa kwenye baadhi ya shughuli na maamuzi ndani ya jamii na sio kuwatenga.


"Lazima ufike muda sasa tukemee hii tabia ya unyanyapaa kwa walemavu ni lazima jamii tuamke na tupaze sauti kupinga tabia za kuwatenga walemavu nchini" alisema Meya huyo 


Hatahivyo,katika kuwatia moyo na kuhamasisha jamii ya watu wenye ulemavu nchini  Meya Maximilian alitoa  mfano wa balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Abdallah Possi ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri hapa nchini kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi ambapo alisema kiongozi huyu ana ulemavu wa Ngozi lakini ameaminiwa na kupewa nafasi na anayatekeleza majukumu yake kama kawaida.


Alimtaja mwanamuziki wa nchini Marekani,Stevie Wonder ambaye ni  mlemavu wa macho ambaye ametamba sana duniani kote kwa utunzi na uimbaji wa nyimbo zinazovutia na kudai pamoja na ulemavu lakini anaimba na kutunga nyimbo kama walio na macho .


Meya Maximilian alitoa mfano mwingine wa  mwanariadha mashuhuri Mlemavu wa Miguu yote miwili nchini Afrika ya Kusini, Oscar Pistorius ambaye amewahi kushida medali katika michuano ya  Olympic na kusema  mifano hiyo ameitoa kuonyesha kuwa ulemavu hauwazuii watu wenye changamoto hiyo kufikia malengo yao waliyojiwekea.


 Alimalizia kwa kutoa wito kwa Jamii ya Watu wenye Usonji kuendelea kujituma katika nyanja mbalimbali bila kukata tamaa pamoja na hali waliyonayo.


Share To:

Post A Comment: