Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo ametilia mkazo umuhimu wa Kilimo Biashara kwa kuondokana na kilimo tumbo yaani kilimo kwa ajili ya chakula pekee.


Katibu Mkuu ameyasema hayo leo jumatatu tarehe 04 Aprili, 2022 jijini Dodoma katika Hafla ya uzinduzi wa Ugawaji wa vitendea kazi kwa maafisa Ugani  nchini, ikiwa ni hatua kuelekea kwenye Ajenda ya 10/30 ya Kilimo ni Biashara.

Mgeni Rasmi Katika Hafla hiyo ni Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akitoa Salam za Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu ameeleza kuwa, "Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 Ukurasa wa 32 na kuendelea, inaeleza kwa undani maendeleo ya Sekta ya Kilimo, na mambo ya msingi ambayo yameelezwa ni Serikali kuhakikisha inasaidia wakulima kutoka kwenye kilimo cha kawaida na cha kujikimu yaani "kilimo tumbo" kwenda kilimo biashara na kilimo cha kisasa".

Ameongeza kuwa, "Lengo la CCM ni kuwafanya wakulima watoke, kwenye maisha duni ya kila siku na majembe begani kwenda kwenye kilimo ambacho kinamkwamua na kuboresha maisha ya mkulima mmoja mmoja na tija ya Taifa kwa ujumla,".

Katibu Mkuu akifafanua zaidi ameeleza kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka vipaumbele kama vile upimaji wa udongo, kuwa na mbegu bora na salama, uzalishaji wenye tija na kutoka kwenye viuagugu kwenda kwenye viautilifu na viuadudu, msukumo katika kuzalisha mbolea isiyo na mdhara kwa udongo na maeneo mengine.

Aidha, Katibu Mkuu kwa niaba ya CCM amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Kilimo Kwa ujumla kwa ubunifu na kutafsiri kilichoandikwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuleta matokeo chanya kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kugawa pikipiki na vitendea kazi vingine ikiwemo vipima afya ya udongo, simu janja kwa maafisa Ugani elfu saba kote nchini zoezi lililofanywa leo na Mhe. Rais Samia.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Wabunge, Viongozi wa sekta binafsi, viongozi wa dini,  Viongozi wa Kimila na Maafisa Ugani kote nchini.

Imetolewa na;

Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI 

Share To:

Post A Comment: