Hili ni zao la biashara, pia chakula. Zao hili hustawi na kulimwa kwa wingi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Pwani.

Matumizi:  Matango hutumika kama tunda, ijapokuwa ni aina ya mboga na huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Pia, tango linaweza kutumiwa kama saladi wakati wa mlo.

Hali ya hewa: Matango hustawi kwenye hali ya joto, hali kadhali kwenye sehemu yenye joto kidogo pia hustawi. Matango yanahitaji joto wastani wa nyuzi joto 20°C – 25°C. Zao hili pia huhitaji maji kwa wingi, ingawa unyevu ukizidi husababisha magonjwa kwenye majani na maua.

Udongo:  Kwa ustawi mzuri wa matango, udongo unatakiwa kuwa na rutuba ya kutosha, na chachu ya kuanzia 5.5 hadi 6.7, mwinuko unaotakiwa ni kuanzia mita 1000-1200 kutoka usawa wa bahari.

Tofauti na ilivyo mazao mengine, matango hayahitaji mwanga mkali sana kwa kuwa husababisha maua dume kuzaliwa, hivyo kuathiri uzalishaji wa idadi ya matunda ya matango. Mwanga kidogo husababisha maua jike kuchanua kwa wingi kuongeza kiwango cha mazao. Mwanga unapokuwa mwingi, inabidi kutumia neti au aina nyingine ya vizuizi ili kupunguza mwanga, ambapo pia itasaidia kulinda mmea dhidi ya upepo mkali ambao unaweza kuharibu maua na matunda, au mmea kwa ujumla.

Kupanda: Mara nyingi matango hupandwa moja kwa moja shambani. Wakulima wengine hupanda kwenye vitalu au makopo na baadae kuhamishia miche inapofikia sentimita 8-12. Endapo mbegu zimepandwa shambani moja kwa moja, inatakiwa ipunguzwe na kubakia mche mmoja tu kwenye kila shimo.

Nafasi: Nafasi kati ya mche na mche ni sentimita 60-70, na nafasi kati mstari na mstari ni sentimita 70-90. Mimea inatakiwa iwekewe miti ili iweze kuzaa matunda mengi na kuepuka kukaa chini ambapo matunda yanaweza kuoza au kuharibiwa na wadudu.

Mbolea:  Mbolea ni muhimu sana, kabla ya kupanda au kuhamisha miche. Mbolea inayoweza kutumika ni samadi au ya viwandani isiyokuwa na madhara kwa mazingira na afya ya binadamu. Baada ya kupanda, tumia mbolea ya maji maji kila baada ya siku 14-21, mpaka mmea uweke matunda.

Palizi: Palizi ni muhimu , ili kuepuka magonjwa na kunyang’anyana chakula kati ya zao na magugu.

Wadudu waharibifu: Wadudu waharibifu wa matango ni pamoja na Vidukari, inzi weupe, na minyoo ya mizizi.

Magonjwa: Magonjwa yaliyozoeleka kushambulia matango ni pamoja na Ukungu, fusari, na magonjwa ya virusi.

Kuvuna:  Matango yanaweza kuwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50-60 na matunda yanatakiwa yawe na urefu wa sentimita 15 mpaka 20. Makadirio ya mavuno ni tani 6 kwa ekari moja.
Share To:

Post A Comment: