Na Seif Mangwangi, Arusha
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ameitaka bodi ya wakurugenzi ya mfuko wa Hifadhi ya Jamii PSSSF kubuni na kuwekeza kwenye miradi yenye tija na uwezo wa kutengeneza ajira nyingi pamoja na kuuingizia mfuko faida.
Pia Waziri huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kutolewa kwa hatifungani kama malipo ya deni la Serikali kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Akizungumza leo Ijumaa Machi 11,2022 alipokuwa akizindua bodi ya Wakurugenzi ya wadhamii ya PSSSF iliyoteuliwa Disemba mwaka jana 2021. Waziri Ndalichako ameelekeza uwekezaji uwe kwenye miradi yenye tija na endelevu na Mfuko uendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kuwekeza kwenye viwanda vyenye uhakika wa kuongeza ajira na vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini.
“Nafahamu mnawekeza katika viwanda, mfano kiwanda cha Karanga (kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro), jana nilivaa viatu vya Karanga, ni vizuri sana, nawapongeza sana. Kiwanda hiki kitasaidia sana wafugaji wetu kuuza ngozi” alifafanua na kuongeza:,
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya kipindi cha mwaka mmoja amewezesha kutoa trilioni 2.17 kwa ajili ya kulipa deni hilo lililodumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi aliyoizindua, Profesa Ndalichako amesema bodi hiyo inapaswa kushauri na kusimamia uwekezaji unaofanywa na Mfuko kwa lengo la kulinda pesa za wanachama.
“Natoa rai kwa Bodi kuhakikisha mnatekeleza majukumu yote. Nawapongeza kwa sababu Mfuko umeendelea kukua, naomba mhakikishe masuala yote ya fedha mnayasimamia vizuri ili tuweze kulipa mafao. Naomba mhakikishe mnawekeza kwenye miradi yenye tija”.
Kwa upande wa watumishi wa PSSSF, Waziri Ndalichako amewataka watumishi wa mfuko huo kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano ili kufikia malengo yaliyopangwa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba amesema katika kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia, mfuko umetekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kuboresha mtandao wa kiofisi kwa kila mkoa na baadhi ya Wilaya zenye ofisi, kuanzisha kituo cha simu za bure kwaajili ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku.
“uwepo wa dawati la malalamiko ofisi zote za PSSSF, PSSSF kiganjani, kwaajili ya wanachama kujihudumia wenyewe kwa simu, popote ulipo mtandaoni, uwepo wa anwani pepe kwaajili ya kupokea hoja mbalimbali na uhakiki wa wastaafu kwa kutumia alama za vidole,”amesema.
Akizungumzia utendaji wa Mfuko CPA Kashimba, alisema tangu kuanzishwa kwake Mfuko unatekeleza majukumu yake vyema chini ya usamimazi wa Bodi ya Wadhamini na kuongeza kuwa changamoto zilizokuwa katika mifuko iliyounganishwa zimefanyiwa kazi na sasa wanachama wa PSSSF wanapata huduma bora kwa kiasi kikubwa.
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini iliyozinduliwa inajumuisha; Mhandisi Musa Iyombe (Mwenyekiti), pamoja nae wajumbe wengine ni; Dkt. Aggrey K. Mlimuka, Bi. Suzan B. Kabogo, CPA Stella E. Katende, Bw. Victor F. Kategere, Bi. Mazoea Mwera, Bw. Thomas C. Manjati, Bw. Said A. Nzori na Bw. Rashid M. Mtima. Bodi ya Wadhamini ya PSSSF imeundwa kwa kuzingatia utatu wa uwakilishi kutoka Serikalini, Wafanyakazi na Waajiri.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Iyombe amesema, “Tunashukuru sana Mhe. Waziri kwa kuja kutufungulia, asante sana. Nakuhakikishia kazi ya Bodi ni kukushauri, sisi kama Bodi tutatekeleza majukumu yetu kwa uaminifu na uadilifu, tupo makini hatutakuangusha.
Hafla ya uzinduzi wa Bodi ilihudhuriwa na; Profesa Jamal Adam Katundu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu ambaye ameitaka bosi hiyo kubwa mfano wa kuigwa dhidi ya bosi zingine kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa maadili.
Post A Comment: