WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) uhakikishe fedha ya mikopo kwa wakulima wadogo zinatumika ipasavyo na kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

 

“Benki ya Maendeleo ya Kilimo izingatie agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kwamba fedha kwa ajili ya mikopo zinatumika ipasavyo, zinawafikia wakulima wengi zaidi wakiwemo wakulima wadogo na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,” amesema.

 

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumatatu, Machi 7, 2022) wakati akizungumza na viongozi na wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa ushirikiano wa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa (Tanzania Inclusive Processor-Producer Partnerships in Dairy - TI3P) kwenye ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

 

Mradi huo unalenga kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maziwa kupitia uhamasishaji wa uwekezaji kutoka sekta ya umma na sekta binafsi kwa kusudi la kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, kuongeza ukusanyaji wa maziwa katika mfumo ulio rasmi, kukuza uwezo wa viwanda katika uchakataji wa maziwa, na kupanua wigo wa soko la bidhaa za maziwa.

 

Aidha Waziri Mkuu ameitaka Benki hiyo ihakikishe kuwa inaweka kipaumbele katika kuwafikia wakulima wadogo, wenye biashara ndogo na za kati zinazojihushisha na kilimo, ufugaji na uvuvi yakiwemo makundi maalum ya wanawake na vijana ili kuchagiza ukuaji wa mnyororo mzima wa thamani katika kilimo, kukuza ajira na kipato cha Mtanzania wa kawaida.

 

“TADB wekeni utaratibu wa kuwa riba na masharti nafuu kwa Watanzania ili wengi waweze kunufaika na kutoa kipaumbele kupitia mikopo ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu,” amesisitiza.

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi iimarishe eneo la utafiti hasa kwenye vyuo vya utafiti kwa kufanya tafiti ambazo zitatoa suluhisho kwa changamoto katika sekta ya mifugo ili kuongeza ubora na wingi maziwa.

 

“Wizara iimarishe na kuboresha koosafu za ng’ombe ili kupata ng’ombe bora wa maziwa kwa njia ya uhamilishaji kwa kutumia chupa (Artificial Insermination) na uzalishaji kwa njia ya kiiini tete (embryo transfer).”

 

Ameitaka wizara hiyo endelee kuhamasisha unywaji wa maziwa maofisini na kushirikiana na TAMISEMI kuendeleza Mpango wa Unywaji wa Maziwa Shuleni. “Tuanzishe kampeni maalum za unywaji maziwa na hili zoezi liwe endelevu,” amesisitiza.

 

Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Maafisa Mifugo katika kila wilaya waanzishe vituo vya kukusanyia maziwa ili kuimarisha soko la maziwa na kutaka wananchi waelekezwe masoko yalipo.

 

Waziri Mkuu alishuhudia uwekaji saini wa makubaliano yakayowezesha ufanikishaji wa mradi huo baina ya Benki ya Kilimo (TADB) na taasisi ya Bill & Melinda Gates wenye thamani ya dola za Marekani milioni saba.

 

Mapema, akielezea mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege alisema mradi huo wa miaka mitatu unalenga kuwafikia wafugaji 100,000 na viwanda kati ya 9 hadi 12 ambavyo vitasaidiwa kuandaa mikakati thabiti ya kibiashara na masoko ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa maziwa na uhamasishaji wa unywaji wa maziwa ikiwepo programu za unywaji maziwa mashuleni.

 

“Ukiondoa dola za Marekani milioni saba za Bill and Melinda Gates Foundation, napenda kuishukuru Serikali kwa kutukubalia ombi letu la kufanikisha kiasi cha dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uwekezaji katika mradi huu, ili kuweza kuleta matokeo makubwa zaidi.”

 

Alisema tangu Februari 2018 hadi sasa, TADB imefanikiwa kuwekeza kiasi cha sh. bilioni 16.4 kwenye sekta hiyo na kwamba imeweza kukopesha moja kwa moja sh. bilioni 15.6 kwa wafugaji na viwanda vya maziwa.

 

“Kati ya sh. bilioni 15.6, tumekopesha shilingi bilioni 14 kwa viwanda sita vya uchakataji na uzalishaji maziwa, shilingi milioni 547 kwa vyama vya ushirika (AMCOS) sita na  shilingi milioni 776 kwa wanufaika wengine kama makampuni na biashara ndogo za kati (SMEs) zinazojishughulisha na ufugaji, usindikaji na uzalishaji wa maziwa,” na kuitaja mikoa iliyonufaika kuwa ni Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Mara, Njombe, Tanga na Shinyanga.

 

Naye mwakilishi wa Bill and Melinda Gates Foundation (BMGF), Bi. Marcela McClatchey alisema taasisi hiyo imetoa dola za marekani milioni saba ili kuendeleza sekta ya wazalishaji na wasindikaji wa maziwa.


“Tumelenga kuwawezesha Watanzania ambao ni wakulima na wenye makampuni kukua na kufanikiwa katika sekta ya uzalishaji na usindikaji wa maziwa.”


 


Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Adam Malima alisema ana imani mradi huo wa TI3P utawasaidia wafugaji wa mikoa mbalimbali nchini kufuga kisasa na kuzalisha maziwa kwa wingi zaidi. “Kwa upande wetu tunajipanga kutoka kwenye ufugaji wa makundi makubwa ya ng’ombe na kuwa nao wachache ambao watafugwa kibiashara.”


 

 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: