OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amebaini upotevu wa fedha na matumizi yasiyosahihi  ya kiasi cha shilingi milioni 231.84 katika ujenzi wa shule ya  Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula, miundombinu ya jiko na bweni.


Waziri Bashungwa amebaini hayo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya Mvomero mkoani Morogoro  na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Hassan Njama  kutoa ufafanuzi wa fedha hizo.


“Nikiwa hapa shule ya Sekondari Sokoine nigependa kuona na kujiridhisha fedha zilizoletwa na Serikali Milioni 700 ambazo zilitakiwa kujenga bwalo la chakula, bweni na jiko kama zimetumika kulingana na mujibu wa BoQ” amaesema Bashungwa


Bashungwa amesema kutokana na tathmini iliyofanywa na Tume maalum ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za ukamilishaji wa miundumbinu  katika shule ya Sokoine imebaini upotevu, matumizi yasiyo sahihi ya shilingi milioni 231.84


Amefafanua kuwa kulingana na taarifa iliyotolewa gharama halisi ya kazi iliyofanyika ni  shilingi milioni 468.15 zikilinganishwa na fedha zilizopokelewa milioni 700 hivyo ilitakiwa kiasi cha shilingi milioni 231. 84 kiwe kimebaki na kutaka kupata maelezo ya kina fedha hiyo nyingine ilipo.


Aidha, Wakati akikagua ujenzi wa jengo la huduma ya dharura katika Hospitali ya wilaya Mvomero hakuridhishwa na kuchelewa kwa kuanza ujenzi huo ambapo Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 300 kutekeleza mradi huo na kumuagiza kuanza ujenzi ndani ya siku 7.


Vile vile, Bashungwa alikagua ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Mlali ambayo imekamilika lakini haijaanza kutoa huduma na kumuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kusaidia upatikanaji wa vifaa, vitendanishi na vifaa tiba kwenye vituo va afya vilivyokamilisha ujenzi.

Share To:

Post A Comment: