Na Englibert Kayombo WAF - Dodoma.


Serikali kupitia Wizara ya Afya imewataka watendaji wa Sekta ya Afya nchini kuboresha usimamizi wa shughuli za uhamasishaji wa uchangiaji wa damu salama ili kukidhi mahitaji ya damu salama nchini.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel mapema leo aliposhiriki kwenye Kikaokazi cha kujadili uboreshaji wa uendeshaji wa usimamizi wa huduma za damu salama nchini kilichowakutanisha kwa pamoja Waganga Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara pamoja na Watendaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama 


"Tumeona kuna shida kubwa ya damu, damu haiuzwi wala kutengenezwa, ili tupate damu ni lazima tuhamasishe watu watoe damu" amesema Dkt Mollel na kuongezea kuwa wamekutana kwa pamoja ili wajadiliane na kuja mikakati bora ya kuboresha ukusanyaji wa damu salama pamoja na kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu katika kuhamasiaha zaidi jamii kuchangia damu.


Dkt. Mollel amesema kuwa kipaumbele cha Wizara ya Afya ni kuboresha huduma za afya nchini kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na iliyo bora hivyo upatikanaji wa damu salama ni ajenga muhimu katika kufikia malengo ya Wizara.


"Tubadilishane uzoefu wa namna wataalam wenzetu kwenye kanda zetu 8 za damu salama wanavyofanya kazi ikiwa ni pamoja na kusaidiana rasilimali zilizopo na kuhakikisha kuwa tunakusanya damu salama kwa kiwango kikubwa zaidi" amesema Dkt. Mollel.


Aidha Dkt. mollel ameushauri Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuendelea kutambua mchango wa wachangiaji damu na kuwa nao karibu ikiwa ni pamoja na kuwasadia pindi wanapohitaji huduma za damu salama.


Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt. Magdalena Lyimo amesema kuwa lengo la 

Serikali ni kuhakikisha huduma za damu salama zinapatikana wakati wote na ili kufanikisha azma ya Serikali wanapaswa kukusanya damu salama ili kutosheleza mahitaji ya nchi.


"Damu Salama ni nguzo muhimu ya utoaji wa huduma za afya, Ili kukidhi mahitaji ya damu hapa nchini tunapaswa kukusanya chupa 550,000 za damu sawa na asilimia moja ya idadi ya wananchi" amesema Dkt. Lyimo.

Dkt. Lyimo amesema kwa Mwaka 2020/21 waliweza kukusanya chupa 330,000 sawa na asilimia 60 ya mahitaji hivyo kuwa na uhaba wa asilimia 40 sawa na chupa 220,000 za damu.


"Kikao hiki kimeitishwa sasa ili tuje kujadiliana na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunaziba hilo pengo la asilimia 40 na kufikisha idadi ya chupa 550,000 za damu kwa kuongeza hamasa zaidi ya uchangiaji damu pamoja na kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchangia damu" amefafanua Dkt. Lyimo.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu ameahidi kuboresha zaidi usimamizi wa mikakati iliyowekwa ya ukusanyaji damu na kuwataka wataalam wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya kufanyia kazi maelekezo yote yanayotolewa na Viongozi wa Wizara ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa wateja na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora.

Share To:

Post A Comment: