Matilda Kasanga na Nuru Mwasampeta
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), DKt. Stephan Ngailo amewataka viongozi na wana vikundi vya wakulima mkoa wa Lindi kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya mbolea kwa kilimo chenye tija.
Dkt. Ngailo ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kukagua mashamba ya mfano yaliyolenga kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea bora kwa wakati kwa shughuli za kilimo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Aidha, Dkt. Ngailo amewataka wakulima wa mazao ya mahindi kufuata kanuni zote za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchagua shamba, kuandaa shamba kwa wakati, kupanda kwa kutumia mbolea sahihi ya kupandia na kwa wakati, kuweka mbolea ya kukuzia na kupalilia kwa wakati.
"Shamba likifuata kanuni zote za kilimo huwa na matokeo mazuri na hivyo kuongeza tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla" Dkt. Ngailo alisisitiza.
Dkt. Ngailo aliongeza kuwa, kufuatia kutokuwepo kwa matumizi ya mbolea kwa wakulima katika mikoa ya Lindi na Mtwara, mamlaka iliona vyema kufanya uhamasishaji kwa njia ya kuanzisha mashamba ya mfano ambayo vikundi vya wakulima vinashiriki kikamilifu kuanzia msimu wa kupanda mpaka msimu wa mavuno ili kujionea kila hatua zi avyokwenda na kupata ujuzi.
Pamoja na kuanzisha mashamba ya mfano mamlaka imewawezesha wanakikundi mmoja mmoja ili kwenda kutumia kwenye mashamba yao binafsi ili wananchi wengine waweze kujifunza.
Amesema, wakulima wakihamasika kutumia mbolea suala la njaa litakuwa historia kwa mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Ruangwa.
"Tutatokomeza njaa lakini pia kipato cha mkulima mmoja mmoja kitaongezeka na kupunguza umaskini, Kachime alikazia.
Aidha, Kachime aliishukuru mamlaka kwa kuanzisha mashamba ya mfano katika kata anayoisimamia na kueleza wakulima wamehamasika na kuona utofauti mkubwa kati ya shamba lililopandwa kwa mbolea na lisilotumia mbolea.
Amesema, tangu kuanza kwa uhamasishaji huo wakulima 51 wameweza kujifunza namna bora ya kutumia mbolea na kumi miongoni mwao walihamasika kutumia mbolea.
"Tuiombe serikali iendelee kutoa hamasa kwa miaka 3 mfululizo ili kuhamasisha wakulima wengi zaidi waweze kutumia mbolea na kuachana na kilimo bibi (kilimo cha kutotumia mbolea).
Amesema, kata ya Mnacho ni kata inayotegemewa kwa kuzalisha chakula kwa wingi hivyo uhamasishaji wa mbolea utaongeza tija zaidi.
Kwa upande wake, Said Mnangona Afisa kilimo Kata ya chigugu Masasi DC alieleza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imeongeza tija kwake na kwa wakulima wengine kwani katika heka moja na nusu aliyolima anatarajia kuvuna gunia 30 za mahindi tofauti na awali alipokuwa akivuna chini ya gunia nane za mahindi.
Mzee Rashid Mandumba mwanakikundi wa jitegemee anasema huko awali alikuwa hatumii mbolea kulingana na desturi na mazoea na kukiri kuwa uhamasishaji wa matumizi ya mbolea umeleta tija kwake na jamii yake kwa ujumla.
Amesema mbolea inawasaidia kulima eneo dogo lakini wanapata matokeo na kipato kikubwa kuliko kulima eneo kubwa bila mbolea na kuambulia hasara pamoja na kupoteza nguvu.
Ziara hii ni hatua ya maandalizi kuelekea siku ya mkulima yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea inayotarajia kufikia kilele mwezi Aprili 2022 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Post A Comment: