Na. Angela Msimbira TAMISEMI
Wanawake wa Mkoa wa Dodoma wafanya harambee katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake na kuchangia kiasi cha shilingi milioni 17 kwa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam(JAI) wanaojishughukisha na utoaji wa huduma za chakula kwa wagonjwa wasio na uwezo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Akiongoza harambee hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka amesema, fedha taslim zilizopatikana ni kiasi cha shilingi milioni 6, ahadi milioni 11, taulo za kike pamoja na chakula.
Mhe. Mtaka amewataka wanawake wa Mkoa wa Dodoma kutumia maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka kusaidia vikundi vinavyojitoa kwa ajili ya kusaidia jamii ili vikundi hivyo viweze kusonga mbele katika suala zima la utoaji huduma ya kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii.
“Tuwekeze kwenye vikundi vyenye tija ambavyo vimejitoa kwa ajili ya kusaidia wananchi wetu ambao wanauhitaji, hawana uwezi na maskini kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiwekea hazina mbinguni, nawaagiza wanawake wote kufanya kitu cha tofauti katika maadhimisho yenu ya wanawake nchini” amesema Mtaka
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe.Simon Chacha amewasihi wanawake kuwa na malezi mazuri kwa watoto wao bila kuwaachia wasaidizi wa ndani pekee, kwa kuwa wanawake ndio walezi wakubwa ndani ya familia.
Akitoa risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Dodoma Bi. Mary Barnabas ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wanawake kupata mkopo na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Aidha, maadhimisho ya sherehe ya wanawake kwa Mkoa wa Dodoma yalifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu “ Kizazi cha haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu Tujitokeze kuhesabiwa”
Post A Comment: