Diwani wa Kata ya Magila- Gereza katika Halmashauri ya
Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mwajuma Kitumpa (wa tatu kushoto) akiwa
na ndoo yenye maji kichwani, mara baada ya kukabidhiwa mradi wa Kisima
cha Maji Shule ya Msingi Gereza na Taasisi ya Kidini ya DirectAid
Society ya jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa).
Na Yusuph Mussa, Korogwe
Na Yusuph Mussa, Korogwe
WALIMU,
wazazi, wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Magila- Gereza pamoja na
vitongoji vyake, wanatoa shukrani kwa Shirika la Kidini la DirectAid
Society kwa kuweza kuwapatia mradi mkubwa wa maji utakaoweza kusaidia
zaidi ya wanafunzi 656 pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalumu 52
jumla yao wakiwa 708 katika Shule ya Msingi Gereza, na wakazi waishio
karibu na shule hiyo wapatao 5,040.
Hayo
yalisemwa Machi 2, 2022 na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gereza,
iliyopo Kata ya Magila- Gereza, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Rehema
Kiondo. Ni kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa kisima hicho kilichojengwa
shuleni hapo kwa gharama ya sh. milioni 10.
"Jambo
hili ni kubwa sana kwani ni muda mrefu wanafunzi walikuwa wakisumbuka
kubeba ndoo na vidumu vya maji kila siku kwa ajili ya usafi wa majengo
ya shule, kupikia uji pamoja na usafi wa vyoo. Vile vile tunamshukuru
diwani wetu (Diwani wa Kata ya Magila- Gereza, Mwajuma Kitumpa) kwa
usimamizi na uhamasishaji wa jamii na usimamizi makini tangu katika
mchakato mzima wa upatikanaji wa mradi huu.
"Kisima
hiki kitasaidia kwa kuondoa usumbufu huo kwa wanafunzi, kwani maji haya
yatakuwa yanapatikana muda wote. Tunaahidi kutunza mradi huu na vifaa
vyote mlivyotupatia ili viweze kutumika kwa muda mrefu. Hatuna maneno
mazuri ya kuzungumza zaidi ya kuwashukuru na kuwaombea Mwenyezi Mungu
awazidishie pale mlipopunguza basi apajaze zaidi na zaidi" alisema
Kiondo.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Magila- Gereza Shaaban Kitumpa alisema mradi huo ni
mkombozi kwa watoto wa shule hiyo sababu hawatahangaika tena na
vigaloni. Lakini pia wananchi wa kijiji hicho watanufaika kwa mradi huo
kuletwa kijijini hapo.
"Kuna
wenzetu wana shida kama hii, lakin tumepata sisi. Hivyo tuenzi mradi
huu ambao ni mkombozi kwa watoto wetu na jamii. Miundombinu tuilinde kwa
nguvu zote" alisema Kitumpa.
Diwani
wa Kata ya Magila- Gereza Mwajuma Kitumpa aliwashukuru wafadhili hao
kwa mradi huo, na anaomba wafadhili hao kujenga mradi kama huo kwenye
vijiji vya Mgobe, Kalekwa na Kitongoji cha Kiloza, kwani kitongoji hicho
mahitaji yake ya maji ni makubwa kutokana na kuwepo kwa gulio siku ya
Ijumaa, na gulio dogo Jumanne, huku idadi ya watu ikiwa kubwa.
Kitumpa
pia aliomba wafadhili hao kuwaongezea nguvu ujenzi wa Zahanati ya
Kijiji cha Magila- Gereza, kwani hadi sasa imegharimu sh. milioni 25 kwa
nguvu za wananchi wakisaidiwa na Mfuko wa Jimbo ambao umetoa sh.
milioni mbili kwa ajili ya saruji na mabati 120 yaliyoezeka zahanati
hiyo, huku wafadhili wenye hoteli kubwa kwenye kata hiyo Kilimanjaro na
Rock hill, wakisaidiana na wananchi kufikia hatua hiyo.
"Tukiweza
kupata sh. milioni 50, tutaweza kukamilisha zahanati hii ambayo itakuwa
pia ni tegemeo hata kwa vitongoji vilivyopo kata za jirani za Mswaha-
Darajani na Lutindi na Lewa. Eneo hili lipo barabara kuu ya Arusha- Dar
es Salaam, hivyo kukiwa na huduma nzuri kutasaidia watu wanaopata ajali
kama ilivyotokea hivi karibuni" alisema Diwani Kitumpa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Miradi ya Shirika hilo Mkoa wa Tanga ambalo Makao Makuu
yake yapo Dar es Salaam, na mfadhili wake yupo nchini Qatar, Mohamed
Mohamed, alisema miradi wanayotekeleza kwa sasa ni ya mwaka 2021, hivyo
katika miradi ya mwaka 2022, wanaweza kuongeza visima vingine kwa kata
hiyo ya Magila- Gereza.
"Mpaka
sasa kwa Mkoa wa Tanga tumetumia sh. milioni 180 kwa ajili ya uchimbaji
wa visima. Kwenye Wilaya ya Korogwe tumechimba visima vinane vyenye
thamani ya sh. milioni 80, ambapo kila kisima kimoja kimegharimu sh.
milioni 10. Visima hivyo ni Mtonga, Bagamoyo, Kwakombo, Mandela, Segera-
Mashine, Old- Korogwe, Kwasunga, na Magila- Gereza.
"Tutazunguka
kuona wenye mahitaji zaidi. Kata ya Magila- Gereza ina vijiji vingi
havina maji. Tuna uwezo wa kusaidia visima vingine kwa mwaka 2022 baada
ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. DirectAid Society ni mdau wa Serikali,
hivyo tupo kuona huduma za maji na mahitaji mengine yanaifikia jamii"
alisema Mohamed ambaye ni raia kutoka Misri.
MWISHO.
Post A Comment: