Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume  ya kurekebisha sheria Tanzania,  Bw. Khalist Luanda akiwasilisha mada kuhusu maisha baada ya kustaafu katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mbeya, katika baraza la wafanyakazi lililofanyika leo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, Bw. Luanda akieleza mikakati mbalimbali walijiowekea ili kufanikisha malengo ya Tume hiyo.

Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wakifuatilia mawasilisho mabalimbali.

Dereva wa Tume hiyo,  Wense Evadi  akichangia mada.

Mchumi  kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania,  Bi Fatma  Alawi akiwasilisha mada kuhusu mikakati ya miaka mitano inayohusu maendeleo ya Tume.


Na Bashiri Salum, Mbeya 


Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania, imefanya tathmini ya utekelezaji wa sheria katika sekta mbalimbali zikiwemo sheria ya adhabu mbadala, sheria ya sekta ya utalii, na Sheria ya mifugo na uvuvi  lengo likiwa ni kubaini changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake na kuzifanyia tathmini kama malengo yaliyokusudiwa wakati wa kutungwa kwa sheria hizo yamefikiwa. 

Akifafanua leo katika kikao cha Baraza la wafanyakazi  kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa BOT Tawi la Mbeya  katika wasilisho lililotolewa katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume  Bwana Khalist Michael Luanda akabainisha kwamba tathimini hiyo imefanyika kwa kupitia sheria nyingi zinazotumika katika sekta mbalimbali ambapo Tume inatarajia kukamilisha taarifa nne (4) za tathmini ya utekelezaji wa sheria.

Aidha Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza mikakati ya Tume katika kuimarisha mawasiliano kwa kutumia vyombo vya habari  ili kuitangaza taasisi hiyo ambapo kwa sasa wanajipanga kuandaa na kurusha vipindi vya redio na  runinga kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Hata hivyo Bwana Luanda amebainisha kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria imejipanga kutoa elimu kupitia vyombo vya habari  juu ya Ushiriki wa wananchi katika mchakato wa maboresho ya Sheria  hapa nchini .

“Sheria nyingine ambazo Tume imetoa elimu ni Sheria ya Mtoto, Sheria za Ajira Tanzania, Sheria za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi na Haki za walaji”.  Alisisitiza katibu Mtendaji  Khalist Luanda.

Naye Mchumi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bi Fatma Saidi Alawi  wakati wa wasilisho lake kuhusu mikakati ya miaka mitano ya  Taasisi hiyo amesema kipindi cha Julai, 2021 hadi Februari, 2022, Tume imechambua hukumu hamsini (50) za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania na kuzibainisha Kanuni za Kisheria (Legal principles) mbalimbali zilizotumika katika kufanya uamuzi.

Aidha Bi Fatma ametoa  wito kwa wadau mbalimbali  wanaohitaji kutumia Kanuni hizo kutembelea  tovuti ya Tume kwa ajili ya kurahisisha watumiaji kufuatilia maendeleo ya Sheria mbalimbali kupitia maamuzi ya Mahakama.

Akiendelea na wasilisho lake Bi Fatma akafafanua kwamba Katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Februari, 2022, Tume imeshiriki katika kutafsiri sheria 17 zinazosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.  

Akimalizia wasilisho lake Bi Fatma anasema kwamba Tume  imeandaa Miongozo ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji.

Hata hivyo baraza la wafanyakazi  limehitimishwa leo  baada ya wajumbe kutumia siku mbili kujadili mambo mbalimbali ya kiutumishi pamoja na mikakati ya kuboresha uendeshaji wa Taasisi hiyo. 


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: