Na Joachim Nyambo,Mbeya.
MAMLAKA ya dawa na vifaa tiba(TMDA) imeisihi jamii kutokuwa na matumizi holela ya dawa ya kuzuia mimba aina ya P2 kwakuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya nyanda za juu Kusini,Anitha Mshighati alisema wanawake hawapaswi kutumia P2 kama karanga na badala yake wanapaswa kuzitumia kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Anitha amesema mtumiaji wa P2 anashauriwa kutomeza dawa hizo mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja huku akizingatia kuwa matumizi ya dawa hizo ni ya wakati wa dharula pekee kwaajili ya kumsaidia mwanamke kutopata ujauzito ambao hakuutarajia.
Ametaja dharula ambazo humfanya mwanamke kutumia aina hiyo ya dawa zilizo kwenye kundi la dawa za uzazi wa mpango kuwa ni pamoja na mwanamke kufanya tendo la ndoa katika siku ambazo ni hatarishi kwa kupata ujauzito kwa mfano kondomu kupasuka wakati wa tendo hilo.
Sababu nyingine ni mwanamke anayetumia vidonge vya uzazi wa mpango anapofanya tendo la kujamiiana akiwa amesahau kumeza dozi yake au iwapo mwanamke amebakwa.
“Mtumiaji wa dawa hii anatakiwa kumeza kidonge kimoja tu cha Miligramu 1.5 ndani ya masaa 72 mara tu baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa na mtumiaji hatakiwi kutumia hizi dawa kama karanga.Dawa hizi zinatakiwa kumezwa mara moja tu katika mzunguko wa hedhi..yaani ndani ya mwezi mmoja.” Alisema Anitha.
Amesema iwapo mtumiaji atameza P2 mara mbili au zaidi katika mzunguko mmoja wa hedhi ufanisi wa dawa hiyo utapungua na mhusika anaweza kupata ujauzito.
Kaimu Meneja huyo ameyataja madhara yhatokanayo na matumizi holela ya P2 kuwa ni pamoja na kubadili mzunguko wa hedhi kwa mtumiaji,kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi,kupata saratani ya kizazi,kichefuchefu na kutapika na pia dawa kushindwa kufanya kazi na mwanamke kupata ujauzito.
Ametaja hatua zinazochukuliwa na TMDA baada ya kufanya tathmini ya madhara hayo kuwa ni pamoja na kuagiza watengenezaji wa dawa kuainisha madhara yanayojitokeza kwenye vikaratasi ambatanishi vya dawa zao iwapo hayakuainishwa awali.
Hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuzibadilishia kundi la dawa la awali na kuziingiza kwenye kundi la dawa zinazohitaji udhibiti maalumu,kuishauri Wizara ya Afya kubadilisha sera ya dawa husika ndani ya nchi,kutoa taarifa za madhara yanayotokea kwa Shirika la Afya duniani(WHO) kupitia mtandao wa Shirika hilo ujulikanao kama Vigiflow.
Pia TMDA imeongeza vikwazo kwenye upatikanaji wa dawa husika,kudhibiti uingizwaji wa dawa husika nchini kwa kutoa vibali vya kuingiza dawa nchini na pia kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya dawa.
Aliwasihi wataalamu wa dawa na afya kwa ujumla kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za matumizi holela ya P2 kwa afya hususani kwa vijana kwakuwa tafiti za kisayansi zimethibitisha kuwa dawa hizo ni salama na fanisi kwa matumizi ya dharula pekee.
“Hivyo mwanamke anayetumia mara kwa mara ni vyema akaenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupatiwa njia sahihi ya uzazi wa mpango kama vidonge,kitanzi,kijiti au kondomu.”
“Pia mwanamke anapaswa kuomba ushauri kabla ya kumeza dawa hizi ikiwemo kumfahamisha mfamasia iwapo kuna dawa nyingine anazotumia ili apatiwe ushauri sahihi.” Alissisitiza.
CAPTION-Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Anitha Mshighati akitoa ufafanuzi juu ya matumizi yaliyo sahihi kwa dawa za kuzuia mimba aina ya P2.
Post A Comment: