Washiriki
wa Mafunzo hayo wakifuatilia Hotuba za ufunguzi. Mafunzo yakiendelea.
Washiriki
wa Mafunzo hayo wakifuatilia Hotuba za ufunguzi. | Mafunzo yakiendelea |
Washiriki
wa Mafunzo hayo wakifuatilia Hotuba za ufunguzi.
Na Calvin
Gwabara – Dar es salaam.
MAAFISA Mawasiliano na Waandishi wa habari wametakiwa kutumia
taaluma zao kufikisha matokeo ya tafiti na vumbuzi mbalimbali zinazozalishwa na
watafiti nchini kwa Wakulima na wafugaji ili zisaidie kutatua changamoto
zinazoikabili sekta hiyo ili kuinua uchumi wa watu na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Meneja wa kituo cha Utafiti wa Kilimo
cha Mikocheni Dkt. Joseph Ndunguru wakati akifungua mafunzo ya kitaifa ya siku
nne ya kuwajengea uwezo Maafisa mawasiliano, Wagani na Waandishi wa habari namna
ya kuchakata matokeo ya Tafiti na kuwafikishia walengwa sambamba na kufuatilia na
kutoa taarifa za utekelezaji wa maazimio ya Malabo ulioandaliwa na Taasisi ya
Uratibu wa Tafiti za Kilimo (CCARDESA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo Tanzania (TARI).
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa maafisa mawasiliano hawa
kutoka vituo vyote vya utafiti nchini, Wizara ya Kilimo, Wizara ya mifugo na
Uvuvi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mamlaka ya Hali ya Hewa pamoja na
Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari maana wana jukumu kubwa la
kuhakikisha wanatafsiri matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi na kuwafikishia
walengwa na kwa kufanya hivyo kutasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija na
pia kusaidia kufikia malengo ya Maazimio ya Malabo” alisema Dkt. Ndunguru.
Aidha amefafanua kuwa kupitia mafunzo hayo kutawawezesha
kujua Maazimio saba ya Malabo na hivyo kuchochea Serikali kutimiza malengo yake
ya kutenga asilimia kumi ya Pato la taifa kuingiza kwenye kilimo na ushiriki wa
wadau wengine katika kusaidia kuinua kilimo na kuinua uchumi wa jamii na taifa.
Dkt. Ndunguru amesema zaidi ya asilimia 55 ya Waafrika
wamejiajiri kwenye sekta ya kilimo lakini bado kilimo hakijatoa mchango unaokusudiwa katika kuinua pato la
taifa na hii ni kutokana na sababu mbalimbali ambazo zingine tayari sababu hizo
majibu yake yamepatikana kupitia tafiti za kisayansi lakini hazijawafikia
walengwa.
Kwa upande wake Afisa Programu ya CAADP -XP4 kutoka CCARDESA Bi.
Futh Magagula ameipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya kwanza kutekeleza
makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa mwisho uliofanyika Afrika kusini kwa
kufanya mafunzo haya kwa wataalamu hawa wa mawasiliano ili kufahamu mchango wao
katika kusaidia utekelezaji wa maazimio ya Malabo.
“Hii inaonyesha kuwa Tanzania inazingatia na kuyachukulia
umuhimu maazimio ya Malabo lakini pia CCARDESA inazingatia sana swala la
usimamizi wa maarifa kwani ni sehemu ya maeneo muhimu katika mpango mkakati
wake wa muda mrefu” alieleza Bi. Futh.
Ameendelea kusema kuwa
Programu ya CAADP -XP4 inaendelea kusaidia nchi za ukanda wa SADC kuweza
kufikia maazimio ya Malabo hivyo mafunzo hayo ya kitaifa yana umuhimu mkubwa
kwa CCARDESA kwa ujumla.
Bi. Magagula ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kufadhili
Programu ya CAADP -XP4 na kuwezesha kufanikishwa kwa mafunzo haya muhimu pamoja
na IFAD kwa kusaidia masuala ya kitaalamu.
Nae Meneja wa Mawasiliano na
menejimenti ya Maarifa kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Richard
Kasuga amesema mafunzo haya ni moja ya mikakati ya kuhakikisha matokeo ya
tafiti yanawafikia wakulima kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Kitaifa, Kikanda
na kimataifa wamekuwa wakishirikiana kujenga katika masuala ya menejimenti ya maarifa
na mawasiliano.
“Mafunzo haya yaliyoandaliwa kwa
Tanzania ni kuhakikisha tunajenga uwezo kwa wataalamu wetu ili waweze kuchakata
na kuweza kusambaza taarifa hususani matokeo ya utafiti ili yaweze kuwafikia
walengwa mbalimbali wakiwemo wakulima wasindikaji na wadau wengine muhimu
katika sekta hiyo” alisisitiza Dkt. Kasuga.
Ameongeza kuwa wanafanya hivyo
kwakuwa kama tafiti zinazofanywa na TARI au CCADERSA unaweza kufanya vizuri na
kuwainua Wananchi wa Tanzania basi unaweza pia kusaidia kuinua wananchi wa nchi
nyingine za kusini mwa Afrika kama vile Malawi, Zambia, Zimbabwe na nchi
zingine.
Dkt. Kasuga amesema pamoja na masuala
ya kubadilishana maarifa lakini pia wana shughulika na kutangaza masuala
mbalimbali kama vile utekelezaji wa maazimia ya Malabo utekezaji wake kupitia
taasisi mbalimbali ili yaweze kueleweka kwa Wananchi na wadau ili wananchi
waweze kushirikiana na serikali yao kuhakikisha kilimo kinawaletea maendeleo.
|
Post A Comment: