Na Dotto Mwaibale, Iramba
SHILINGI BILIONI 10 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mwaka mmoja wa uongozi wake zimewezesha kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika Tarafa ya Ndago iliyopo Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda wakati akiwahutubia Wananchi wa Tarafa ya Ndago kwenye mkutano wa hadhara baada ya kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo zilipomaliza kukagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Tarafa hiyo jana.
Mwenda alisema kamati hizo zilifanya ukaguzi wa miradi hiyo ili kuona nini kimefanyika katika mwaka mmoja wa uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi katika Tarafa hiyo.
Aliwataja alioongozana nao kufanya ukaguzi huo kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo na kamati ya siasa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo na timu yake wakiwemo wataalam, Mwenyekiti wa Halmashauri na kamati ya ulinzi na usalama.
Alisema mambo yaliyofanyika katika wilaya hiyo ni mengi na kuwa wamepanga kila Tarafa kati ya nne zilizopo waielezee miradi iliyofanyika ambapo wameanza na Tarafa ya Ndago yenye kata sita ambayo ni kubwa kuliko tarafa zingine zote katika wilaya hiyo ambapo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imetekelezwa miradi yenye thamani ya Sh. 10. Bilioni.
Alisema yeye kama kiongozi mkuu wa Serikali na CCM wameona baada ya kufanya ukaguzi huo waitishe mkutano wa hadhara ili waweze kuwaeleza walichokiona katika miradi hiyo, changamoto zilizopo,inaendeleaje, usimamizi wake upoje, lini itakamilika na watarajie nini.
Alisema miradi ya elimu iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan katika shule za msingi wamekamilisha ujenzi wa darasa moja Shule ya Msingi Senenkwa ambalo limegharimu Sh.11.3 Milioni, ujenzi wa darasa moja Shule ya Msingi Azimio ambapo pia wamepeleka kiasi hicho cha fedha.
Mwenda alisema wamekamilisha ujenzi wa bweni moja katika Shule ya Watoto wenye mahitaji maalumu ya Songambele ambapo wamepeleka Sh.80. Milioni, kumalizia chumba kimoja cha darasa Shule ya Sekondari Mtekente walipeleka Sh.20 Milioni, ujenzi wa chumba kimoja cha darasa Shule ya Sekondari Ulugu walitoa Sh.20 Milioni.
Aliongeza kuwa wamejenga vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Ushora ambapo pia walitoa Sh.40 Milioni, ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Ndulungu tayari tumetoa fedha awamu ya kwanza Sh.470 Milioni na awamu ya pili tunategemea kupokea Sh.130 Milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo ya Sekondari kutaifanya Tarafa nzima ya Ndago kila kata kuwa na shule ya sekondari hivyo ni jambo la kujivunia na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyowafanyia Wana Ndago.
Akizungumzia sekta ya Afya alisema wanajenga Kituo cha Afya Mwanduigembe ambapo Serikali itawapelekea Sh.500 Milioni, ujenzi wa Kituo cha Afya Ulugu kwa gharama ya Sh.500 Milioni tayari wamepokea Sh. 250 Milioni.
Mwenda alisema tangu nchi hii ipate Uhuru Tarafa ya Ndago ilikuwa na kituo kimoja tu cha afya na hicho kilichopo ambacho wanakitumia kilijengwa mwaka 1976 kikiwa ni Zahanati ndogo na ilikuwa kabla hata ya CCM hakijazaliwa lakini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan anajenga vituo viwili vya afya katika kila kata ili ni jambo la kushangilia kwani ni zaidi ya miaka 50 kulikuwa na kituo hicho kimoja tu.
"Ni mwaka mmoja tu wa uongozi wake amefanya hivyo je akimalizia na hiyo miaka yake tisa kuwa madarakani si atajenga vituo vya afya katika kata zote za Wilaya ya Iramba" alisema Mwenda.
Akizungumzia Maji alisema katika mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan wamepelekewa Sh. 465 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji Zinziligi na Sh.730 Mradi wa Maji Kaselya yote ikiwa Tarafa ya Ndago.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Malango alisema wamepeleka Sh.201 Milioni na sasa inafanya kazi, alisema wanafungua barabara kutoka Ulugu, Mang'ole hadi Mpugizi ya kilometa 9.5 kwa gharama ya Sh.765 Milioni.
Alisema wanajenga barabara ya ya kutoka Mtekente, Msansao hadi Ujungu ambapo wametoa Sh.999 Milioni karibu Bilioni moja na mkandarasi anaendelea na kazi, ujenzi wa barabara ya Kibaya, Luzurukulu hadi Kipuma ambayo inajengwa kwa Sh.624 Milioni.
"Hivi ndugu zangu kuna Rais kama Mama Samia ambaye ameweza kutoa hela nyingi kiasi hiki tena katika Tarafa ya Ndago tu na si Wilaya nzima ebu pigeni hesabu ninyi wenyewe" aliuliza Mwenda kwenye mkutano huo huku yakipigwa makofi kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwenda alisema mambo hayo ya maendeleleo hayajafanyika katika kata hiyo pekee bali ni kata zote za wilaya hiyo ya Iramba na kuwa hayo ni baadhi tu kwani hajazungumzia ujenzi wa madarasa ya UVIKO na umeme.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iramba Ashery Samwel alisema wameridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo na aliwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza badala ya kuisubiri Serikali.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi katika wilaya hiyo ambapo aliwaomba wakandarasi kujenga miradi hiyo kwa viwango kulingana na fedha walizolipwa.
Aidha Msengi alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kujenga tabia ya kulipa ushuru wa mazao ili kusaidia wilaya hiyo kukusanya mapato yatakayosaidia kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Diwani wa Kata ya Ndago Ernest Kadege alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wao Dk. Mwigulu Nchemba kwa kufanikisha miradi hiyo katika Tarafa hiyo na jimbo zima la Iramba Magharibi.
Wajumbe wa kamati hiyo wakizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo waliwapongeza viongozi wote wa wilaya hiyo, wakuu wa idara kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha miradi hiyo kutekelezwa miradi hiyo kwa uaminifu kwa ufanisi mkubwa.wakuu wa shule na viongozi waliosimamia fedha za kutekeleza miradi hiyo kwa uaminifu na kuifanikisha.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda alifanikiwa kumaliza mgogoro wa barabara ya kutoka Mtekente kwenda Msansao na Ujungu uliotokana na baadhi ya wananchi kugomea isipite katika mashamba yao lakini baada ya kufanyika kwa mkutano wa hadhara uliongozwa na Mwenda wakiwepo viongozi mbalimbali wananchi hao waliridhia barabara hiyo ipite katika eneo hilo baada ya kuomba wiki moja ya kuondoa mazao yao katika maeneo itakapo pita barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo yao.
Post A Comment: