Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Singida, Mhandisi Patrick Zamba (kushoto) akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati hiyo. |
Muonekano wa tenki la kuhifadhia maji kwenye mradi huo. |
Na Dotto Mwaibale, Singida.
MKUU wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge amesema Serikali imeridhia majengo ya iliyokuwa Hospitali ya Mkoa wa Singida kuwa Hospitali ya Wilaya ya Singida.
Dk. Mahenge aliyasema hayo jana wakati kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida ilipokuwa ikikagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Manispaa ya Singida.
"Serikali tayari imekwisha ridhia majengo hayo kuwa Hospitali ya Wilaya baada ya kukubaliana pande zote Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI), Wizara ya Afya, Mkoa na Wilaya" alisema Mahenge.
Alisema suala lililokuwa bado ni idadi ya majengo yatakayochukuliwa ambayo ni saba ya na sasa jambo linalosubiriwa ni Wizara ya Afya kuwaandikia barua TAMISEMI ya kuwakabidhi majengo hayo.
Wakati huo huo Dk.Mahenge ameiagiza Manispaa ya Singida kutoa haraka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mionzi (X-RAY) katika Kituo cha Afya cha Sokoine ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhajj Juma Killimbah alisema wameridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
"Kwa kweli tunawapongeza kwa kuitendea haki miradi hii ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kuitekeleza," alisema Kilimbah.
Kilimbah alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii badala ya kuisubiri Serikali.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Aliwaomba wananchi kila ilipotekelezwa miradi hiyo kuitunza ili iendelee kuwa na manufaa kwao na taifa.
Killimbah aliziomba taasisi za Serikali kama Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (SUWASA) Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka miundombinu kwenye miradi yote iliyotekelezwa lakini hakuna miundombinu hiyo ukizingatia kuwa miradi hiyo Serikali imetumia fedha nyingi kuikamilisha.
Aidha Killimbah amewaomba waandishi wa habari kuandika habari za maendeleo inayofanywa na Serikali katika halmashauri ili wananchi waweze kuielewa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa fedha nyingi za miradi hiyo.
Pia Killimbah aliziomba halmashauri zote za wilaya mkoani hapa kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili waweze kuandika habari hizo kwa nafasi kubwa kutokana na umuhimu wake katika jamii na nchi kwa ujumla.
Wajumbe wa kamati hiyo wakizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo waliwapongeza viongozi wote wa wilaya hiyo, wakuu wa idara pamoja na wataalamu kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha miradi hiyo kutekelezwa kwa uaminifu na ufanisi mkubwa.
Baadhi ya miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo upanuzi wa Mtandao na huduma ya Majisafi Singida mjini kupitia program ya IFF-OBA ambao gharama yake ni Sh.756,552,453.38 uliopo eneo la Somoku, Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Uhamaka unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.470,000,000 kupitia mradi wa SEQUIP 2021/2022.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Mandewa kinachojengwa kwa fedha za tozo kutoka Serikali Kuu Sh.250,000,000, ujenzi wa Zahanati ya Ititi iliyogharimu Sh.50 Milioni na Ujenzi wa Jengo la Mionzi Kituo cha Afya Sokoine ambao umegharimu Sh.120,333,4000.
Post A Comment: