Na Mwandishi Wetu- Zanzibar

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amelipongeza Baraza la Vijana Kibweni kwa kutumia fursa zilizopo nchini kupitia nyanja mbalimbali zikiwemo ushonaji na taasisi za kifedha ili kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri Katambi aliyasema hayo Machi 09,2022 wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya  Katiba na Sheria ilipofanya ziara ya kutembelea na kuona shughuli zinazofanywa na vijana Zanzibar akisema hatua hiyo inaonyesha uthubutu wa vijana kupambana na changamoto ya ajira.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaweka miundo mbinu rafiki kwa vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kujiajiri katika ujasiriamali.

“Nimefurahi sana kupata nafasi ya kutembelea hapa na kuona shughuli mnazozifanya  kama Fuoni na kibondeni kujionea kilimo cha kisasa (Kitalu Nyumba) na kituo cha Radio  Kati Fm  ambayo ni ya  kijamii ya Baraza la Vijana na kiwanda cha  ushonaji, yapo ambayo tumejifunza  na mengine sisi kama Serikali tunayachukua  hasa suala la  uwekezaji kwa vikundi, malezi na mafunzo,” alisema Mhe. Katambi.

Vile vile alitaja shughuli zingine zinazofanywa na baraza hilo kuwa ni  ushonaji, masuala ya  taasisi za kibenki kwa  mifumo ya Simu pamoja na uchomeleaji akisema uamuzi huo unainyesha vijana wako tayari kufanya kazi huku akisisitiza kuendelea kujifunza na kuwa wabunifu kuleta ustawi kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani.

Katika hatua nyingine Mhe. Katambi alieleza kwamba serikali itaendelea kutatua changamoto ya masoko kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na vijana zinapata masoko ya ndani na nje ya Nchi na kuweka kutenga maeneo sahihi kwa ajili ya vijana kufanya biashara zao.

“Nitoe wito kwa Wizara  wizara kuangalia changamoto ya masoko  ya bidhaa zinazozalishwa na vijana hawa jambo ambalo ni la Kiserikali na tumelichukua tunalifanyia kazi, pia kuna maeneo mengine tunatakiwa kuyatenga sababu maeneo mengi ya vijana ambayo tumeyazungukia wana Changamoto zinazofanana kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani ,”alifafanua .

Kwaupande wake Katibu Mkuu Wizara ya , Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Rajabu  alibainisha kwamba wako tayari  kutoa ushirikiano katika  mabaraza la vijana  ili wajikwamue  kiuchumi huku akiishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati hiyo kwa kuwatembelea hatua inayowatia moyo vijana kusonga mbele.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge  ya  Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama  alisema kutokana na yale waliyoyabaini kufuatia ziara hiyo sekretarieti itayafanyia kazi na kupongeza utayari wa vijana kujifunza na kuwajengea uwezo.

Share To:

Post A Comment: