Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete ametoa agizo nchi nzima kwa wavamizi wa maeneo bila kufuata sheria na taratibu kwa kueleza kwamba suala hilo ni uvunjifu wa sheria na ni lazima likome mara moja. 


Mhe. Ridhiwani Kikwete ameyasema hayo leo Jumapili Machi, 06, 2022 wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Diozile kilichopo Chalinze Mkoani Pwani kwenye mkutano wa hadhara ambapo Kijijini hapo pana mgogoro na tatizo kubwa la uvamizi wa maeneo ambapo Wakurya wengi sana wamevamia eneo la Kijiji cha Diozile na kufanya shughuli zao za uchomaji wa mkaa na kilimo kinyume na sheria.


"Hakuna nafasi kwa Watu kwenye nchi yetu kuvamia maeneo bila kufuata sheria. Kumekuwa na watu wanaojulikana kama tegesha ambao wamekuwa wakivamia maeneo na kujitegesha ili baadae waonewe huruma na Serikali ili wapewe maeneo hayo. Jambo hili halikubariki." Alisema Mhe. Ridhiwani.


"Natoa agizo kwa nchi nzima kwamba hakuna nafasi ya kuingia na kuishi sehemu bila kufuata utaratibu. Watu wanaofanya hivi ni wahalifu kama wahalifu wengine. Utaratibu upo wazi kwa mtu anayetaka kuingia na kuishi sehemu ni lazima afuate sheria kwa kujitambulisha kwa Kijiji husika au Serikali ya eneo analotaka kuishi kwasababu Serikali yetu haikatazi mtu yeyote kuishi popote lakini lazima afuate sheria." Alisema Mhe. Ridhiwani.


Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema lazima tumalize migogoro ya ardhi na kudhibiti uvamizi wa maeneo kwasababu nchi haiwezi kuendeshwa kwa watu kuvamia vamia tu maeneo bila kufuata sheria na kuwa na migogoro ya ardhi.


Katika hatua nyingine, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kesho Jumatatu Machi 07, 2022 pale Chalinze patafanyika kikao cha kugawa Hati zaidi ya 300 na kutoa msimamo wa Serikali kuhusu migogoro mbalimbali ya ardhi ikiwemo migogoro aliyoikuta Kijijini hapo Diozile.

Share To:

Post A Comment: