Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameitaka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA) kuhakikisha inaimarisha ukaguzi wa viuatilifu vinavyosambazwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo ili kujiridhisha juu ya ubora wake na usahihi wa matumizi yake.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 29 Machi, 2022 alipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya TPHPA yaliyopo Ngaramtoni, katika Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha na kukagua shughuli za maabara zinazofanywa na Mamlaka juu ya masuala ya Afya ya mimea na Viuatilifu.
"Kwanza nataka kuwapongeza sana TPHPA kwa kufanikiwa kupata ithibati Namba ISO 17025: 2017 kutoka Taasisi ya Kimataifa ya SADCAS ambayo inafanya cheti cha majibu yatokayo katika maabara za TPHPA kutambulika kimataifa na hivyo kuongeza fursa zaidi ya masoko ya mazao yetu nje ya nchi.
Tunataka TPHPA kuwa Kituo cha umahiri cha afya ya mimea na viuatilifu kwa Nchi za SADC na Afrika Mashariki na Kati kwani kuna fursa kubwa ya maabara zenu kutumika na nchi nyingine kutokana na uwepo wa ithibati hiyo inayotambulika kimataifa.
Kumekuwepo na malalamiko ya wakulima kwa baadhi ya viuatilifu kutoua wadudu waharibifu wa mazao na hii inasababishwa, pamoja na sababu zingine, na wafanyabiashara wachache wa pembejeo wasio waaminifu ambao wanachakachua viuatilifu na kuathiri ubora ukwa lengo la kujipatia faida zaidi pasipo kuangalia athari kwa mkulima na afya ya mimea.
Serikali haitavumilia wafanyabiashara wababaishaji wa aina hii ambao wanawasabishia maumivu wakulima, TPHPA hakikisheni mnaimarisha kaguzi zenu za kila siku na mchukue hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa wote watakaobainika kusambaza viuatilifu feki kwa njia zisizo rasmi” Alisema Mavunde
Akitoa maelezo yake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Dkt. Efrem Njau ameahidi kutekeleza maagizo hayo ya Naibu Waziri kwa kuimarisha ukaguzi ambao wamekuwa wakiufanya mara kwa mara kuwabaini wafanyabiashara wa viuatilifu wanaokiuka taratibu, na kutumia fursa hiyo pia kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha shilingi bilioni 1.1 na kuiwezesha Mamlaka kununua mtambo wa kisasa wa kuchambua sampuli za viuatlifu, maji, mbolea na udongo ujulikanao kama MP-AES ili kuongeza ufanisi na kutoa huduma bora kwa wadau wetu ndani na nje ya nchi.
Post A Comment: