.  Waziri Salum, Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali TEA (wa kwanza kulia) akizungumza na Uongozi wa SIDO mkoa wa Mwanza mara baada ya kukagua vifaa vya kujifunzia vilivyonunuliwa na TEA alipofanya ziara kwenye shirika hilo. Kutoka kushoto ni mratibu wa mafunzo Bw. Maneno Maporo na katikati ni Meneja wa SIDO Mkoa wa Mwanza Bw. Bakari Songwe
 Baadhi ya wanafunzi wanaoendelea na mafunzo ya mapishi katika Chuo cha VETA - Mwanza wakiwa darasani. Mafunzo haya ni muendelezo baada ya yale yaliyofadhiliwa na TEA kuisha na kuwa na matokeo chanya kwa jamii.
 Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka TEA Bw. Waziri Salum akikagua taarifa za wanafunzi waliosajiliwa kwa ajili mafunzo ya kuendeleza ujuzi kutoka kwa Mwalimu wa Kitengo cha Ukarimu Bi. Flavian Minde, VETA mkoani Mwanza.
 Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka TEA Bw. Waziri Salum akisisitiza jambo kwa wanafunzi wanaoendelea na mafunzo (hawapo pichani) katika Chuo cha VETA – Mwanza.

Waziri Salum, Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka TEA (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha VETA – Mwanza kuhusu matumizi na utunzaji wa vifaa vilivyonunuliwa kwa ufadhili wa TEA kwa ajili ya Mafunzo. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Muzora Bitesigirwe, Mtaalam wa ufuatiliaji kutoka TEA Bw, Adelard Saduka, na Mratibu wa mafunzo kutoka VETA Bw. Joseph Masaga.

Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bw. Waziri Salum (mwenye koti jeusi) akipewa maelezo kuhusu matumizi ya vifaa vilivyonunuliwa ili kusaidia mafunzo ya ujuzi na mratibu wa mafunzo hayo kutoka SIDO – Mwanza Bw. Maneno Maporo alipokuwa katika ziara ya kimkakati mkoani humo.
Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bw. Waziri Salum (katikati) akikagua baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ufadhili wa TEA ili kuwezesha mafunzo ya ujuzi yaliyotolewa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Mwanza. Mbele yake ni mratibu wa Mafunzo hayo Bw. Maneno Maporo na nyuma yake ni Meneja wa SIDO Mkoa Bw. Bakari Songwe. 


Na Eliafile Solla – TEA


MFUKO wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) umeonyesha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii kutokana na kufadhili mafunzo ya uendelezaji ujuzi kwa kundi la vijana wanaotoka kaya maskini kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) mkoani Mwanza.

Haya yamebainika katika ziara ya Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali wa TEA Bw. Waziri Salum alipotembelea baadhi ya Taasisi zilizonufaika na ufadhili wa SDF kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Mwanza Bw. Muzora Bitesigirwe amesema chuo kilipokea Sh. Milioni 68.6 kutoka TEA kwa ajili ya kugharimia mafunzo ya muda mfupi kwa vijana wanaotoka kaya maskini na mazingira magumu.  Hadi mafunzo yanakamilika, jumla ya vijana 57 wamenufaika kupata ujuzi katika fani za umeme wa majumbani, mabomba, magari, uashi, mapambo na usafi, ushonaji, mapishi pamoja na udereva wa awali.

Mratibu wa mafunzo kutoka chuoni hapo Bw. Joseph Masaga amesema vijana walionufaika na mafunzo hayo sio tu wamepata ujuzi na stadi za kazi bali pia wamewezeshwa kujitambua nafasi zao katika jamii na hivyo kujitoa katika magenge yasiyofaa ambayo baadhi walikuwa wamejiingiza.  

“Baadhi ya waliohitimu mafunzo tayari wamepata ajira za kuendesha magari, pikipiki na bajaji na hivyo kujipatia kipato” amesema Masaga.

Mkurugenzi wa Miradi kutoka TEA Bw.Waziri Salum ameonesha kufurahishwa na matokeo ya mafunzo hayo hasa kwa vile yamesesaidia kubadilisha maisha na tabia za vijana wa Kitanzania ambao wanategemewa na jamii. Alisisitiza mafunzo hayo kuwa endelevu ili yaweze kusadia kundi kubwa la jamii.

Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ni mfuko unaolenga kufadhili programu za mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa wanufaika 30,000 hadi kufikia mwezi Juni 2022.  Mfuko unalenga mafunzo katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni Kilimo na Kilimo - Biashara, Utalii na Huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Nishati. Katika awamu ya kwanza ya mradi huo iliyoanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2018/2019 Taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.1 na awamu ya pili ya mradi Taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 lengo likiwa ni kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: