Na Dotto Mwaibale,
Singida
MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida Mhe. Aysharose Mattembe amewataka Viongozi Wanawake na wanawake wote wa mkoa huo kuendelea kusimama imara, kujiamini kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anachapa kazi kwa bidii na kuonesha uwezo mkubwa wa kuingoza nchi.
Mattembe alisema hayo jana katika maadhimisho ya sikukuu ya Wanawake Duniani ambapo kimkoa yalifanyika Wilaya ya Ikungi.
Mhe.Mattembe ambaye alikuwa mgeni Rasmi alisema Sikukuu hiyo ni siku muhimu sana kwa kuwa ni mahususi kwa kutafakari, kutathmini, kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mwanamke katika nyanja mbalimbali hasa za maendeleo ya Taifa letu na dunia kwa ujumla.
" Dhamira ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ni kutuletea maendeleo, kutuinua kiuchumi na kuhamasisha wawanamke kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa Taifa letu" alisema Mattembe.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassana amefungua milango kwa Wanawake wengi akiwemo Dk.Tulia Ackson ambaye anaweka rekodi ya kuwa mwanamke wa pili kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Stegomena Tax ambaye anaweka rekodi ya kuwa Waziri wa kwanza Mwanamke wa Wizara ya Ulinzi.
Mhe. Mattembe alisema Watanzania tuna kila sababu ya kumuunga mkono na kamwe tusimuangushe na kuwa fursa alizotufungulia tuzitumie vizuri na kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa.
Awali sherehe hizo zilitanguliwa na kupokea mchango na zawadi zilizotolewa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuwachangia watoto wenye mahitaji maalum wa Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko.
Akikabidhi michango hiyo Mhe. Mattembe aliwashukuru wote waliochangia na kuwataka waendelee na moyo huo huo ambao ni Kampuni ya Shanta Mining, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Ikungi, AMREF, Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, UN Women na Ofisi ya Mbunge Aysharose Mattembe.
Pia katika sherehe hizo Mhe. Mattembe alitembelea mabanda ya wajasiriamali na mengine na kujionea bidhaa zinazozalishwa ambalo aliahidi kushirikiana nao na kuwatafutia masoko.
Kwenye sherehe hizo
baadhi ya viongozi mbalimbali walihudhuria walikuwepo wa Chama na Serikali
akiwepo Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mhe.Miraji Mtaturu, Katibu
Tawala wa Mkoa wa Singida (RAS) Doroth Mwaluko, Katiba wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Singida Lucy Shee, Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi Stamili
Dendego, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida
Jonathan Semmit, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga,
Diwani wa Kata ya Ikungi Abel Nkuhwi, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi
Haika Masawe, Katibu Tawala wa wilaya hiyo Winfrida Funto na madiwani wa Viti
Maalumu wa wilaya hiyo.
Post A Comment: