****************************

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Wizara imeandaa kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo wote nchi nzima ili kuwapa mafunzo maalum ya kusimamia na kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuibua vipaji utakaoanzisha ligi kuanzia kwenye ngazi ya Kijiji na mtaa hadi taifa ili kupata timu bora za taifa katika michezo mbalimbali.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Machi 22, 2022 alipokuwa akifungua semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma na amesema kikao hicho kitafanyika Aprili 5-6, 2022 mjini Dodoma na kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa.

Amefafanua kuwa ligi hii ni mpango maalum wa Serikali wa kuendeleza michezo ambao unatekeleza dhana ya kuibua wachezaji kuanzia chini ya mtaa kwa mtaa.

Mbali na kuanzisha ligi hizo Mhe. Mchengerwa ametaja mambo mengine makubwa ambayo wizara yake inakwenda kuyafanya mwezi Aprili kuwa ni pamoja na Wizara inakwenda kuzindua Mpango Mkakati wa michezo ambao utaainisha kazi gani inafanywa lini na nani ili kuboresha michezo.

Aidha, amesema Wizara inakwenda kujenga miundombinu ya kisasa kwenye shule za Sekondari za wavulana na wasichana za Tabora mkoani Tabora ambazo zitatumika kwenye mashindano ya Umiseta na Umitashumta ya mwaka huu.

Kwa upande mwingine amesema tayari Serikali imeshajenga viwanja changamani vya michezo vinne ambapo viwili kwa kanda ya Pwani mkoa wa Dar es Salaam na viwili mkoani Tanga ambapo miundo yote imeshafika zaidi ya asilimia 80.

Kuhusu ujenzi wa kiwanja cha kisasa jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali itahakikisha ujenzi huo unakamilika kabla ya 2025 ambapo amefafanua kuwa hadi sasa michoro imekamilika na tayari wadau kadhaa wamejitokeza kuwekeza.

Mwenyekiti Kamati hiyo Stanslaus Nyongo amemshukuru na kumpongeza Mhe. Waziri kwa ubunifu mkubwa ambapo amesema anaimani kuwa anakwenda kuleta mapinduzi makubwa ambapo ameishauri Wizara kushirikisha wadau wa sekta binafsi kwenye kuwekeza kwenye michezo.

Aidha, ameiomba Wizara kuijengea uwezo Kamati ili iweze kuiomba Serikali kutoa punguzo zaidi kwenye vifaa vya michezo.


Mbunge wa viti maalum na Mjumbe wa Kamati hiyo, Neema Lugangira amepongeza ubunifu wa Wizara wa kuanzisha ligi ya mtaa kwa mtaa ambapo pia amewashauri wajumbe wote wa Kamati kuiomba Serikali kutoa gharama za kupima Uviko na MRI.

Katika semina hiyo Wizara iliwapitisha wajumbe katika mada ya kufanya vizuri katika michezo iliyowasilishwa na Kaimu Katibu wa Baraza la Michezo (BMT) bi Neema Msitha na Mada ya taarifa ya mafanikio ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) Alfred Kidau.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: