Baadhi ya washiriki katika hafla ya utoaji tuzo kwa shule 20 binafsi na Serikali pamoja na walimu wakuu wakiwa katika hafla iliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Ilala Idara ya Elimu Msingi iliyofanyika juzi.
Washiriki wakionesha tuzo zao baada ya kukabidhiwa.


Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo,  Godrick Rutayungururwa akizungumzia tuzo hizo ambazo zimetolewa kama motisha kwa walimu ili kuinua chachu ya ufundishaji.
Hafla ikiendelea.
Tuzo zikioneshwa.
Shamra shamra zikiendelea katika hafla hiyo.
 


Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam


HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imesema  imejipanga kuhakikisha inaongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwafikia  wale wenye mahitaji maalum ili waweze kunufaika na elimu hiyo.

Akizungumza Jijini Dar es salaam  juzi katika hafla ya utoaji tuzo kwa Shule za Msingi za Serikali na Binafsi 20  sambamba na walimu wakuu waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa Tuzo ambazo zimeandaliwa na Umoja wa Viongozi wa Elimu Idara ya Msingi jijini Dar es Salaam, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Sipora Tenga alisema ili kukamilisha mpango huo hadi sasa wametenga shule 15  za Serikali na vituo ambavyo vimekuwa vikitoa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum.

Alisema mpango mkakati huo utawasaidia kupanda kielimu kutoka kiwango cha ufaulu cha sasa ambacho  Halmashauri hiyo imekuwa  namba nne kitaifa na ya pili kimkoa.

Ametaja  shule zinazotoa elimu kwa wenye mahitaji maalum ni  Mtemdeni,Msimbazi Mseto, Mzambarauni, Buguruni Viziwi Uhuru Mchanganyiko, Maarifa, Pugu Kajiungeni, Air Wing, Chanika, Viwege na Tumaini.

Kwa upande wa  vituo vinavyotoa huduma kwa wanafunzi   wagonjwa waliopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mahabusu ya Watoto iliyopo Upanga na wanafunzi wenye magonjwa adimu waliopo nyumbani.

"Katika kutekeleza mkakati huu wa ufaulu na kuwafikia wanafunzi wenye mahitaji maalum kielimu tumepanga walimu ambao wamekuwa wakiwafuata huko walipo na tumeona mafanikio mmoja wa wanufaika hao amefaulu kwa kiwango cha juu kitaifa,'' alisema Sipora.

Alisema Halmashauri hiyo inaendelea na uandikishaji wanafunzi wa darasa la kwanza ambapo hadi kufikia Machi 31 Mwaka huu watakamilisha uandikishaji ambapo kwa sasa 25,695 tayari wameandikishwa.

Amewapongeza walimu hao kwa kuongeza kiwango cha ufaulu  ambapo asilimia ya ufaulu imekuwa ikiongezeka Mwaka hadi Mwaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, N'gwilabuzu Ludigija aliwapongeza walimu hao kwa ufaulu huo na kuwaagiza waendelee kushirikiana kwenye changamoto ili kuzidi kuinyanyua kielimu halmashauri hiyo.

Alisema wamefanya jitihada za kutengeneza miundombinu kadhaa ya kielimu ili kurahisisha utendaji kazi na hatimaye kunyanyuka kidedea kwenye mitihani mbalimbali.

 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, Tabu Shaibu, amewapongeza walimu hao kwa ufaulu wa matokeo yaliyopita na kusema yameenda sambamba na hadhi ya eneo husika.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo,  Godrick Rutayungururwa alisema, tuzo hizo zimetolewa kama motisha kwa walimu hao ili kuinua chachu ya ufundishaji zaidi ambao utanyanyua kiwango cha elimu nchini.

Amezitaja baadhi ya tuzo hizo kuwa ni uongozi,  Sanaa na michezo, taaluma na  utendaji wa heshima.

Rutayungururwa amesema kumetolewa  tuzo  kwa shule za msingi Serikali 10 zilizofanya vizuri na shule 10 binafsi.

Pia alisema tuzo nyingine 36 zimetolewa kwa  Maafisa elimu kata na   Walimu wakuu  tuzo 248 kutoka shule zilizofanya vizuri katika upimaji darasa la nne na la saba.

"Tuzo nyingine 23  zimekwenda  kwa mdhibiti ubora wa shule na umitashumita, tano kwa nyingine Walimu ambao wanafundisha watoto wenye mahitaji maalumu katika hospitali ya Taifa Muhimbili, mahabusu ya watoto na mtoto mwenye tatizo la kiafya anayefundishwa nyumbani.

Aliongeza kuwa  tuzo  nyingine zimetolewa kwa  idala mbalimbali ikiwemo madereva wa idara tuzo  tano, kamati ya huduma ya jamii na uchumi tuzo moja, Afisa elimu mkoa moja, Naibu Meya moja, Mkurungezi , Meya na ofisi nyinginezo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: