Na Ahmed Mahmoud
BUNGE la Afrika Mashariki, (EALA) wamepitisha muswada wa kutambua Umoja wa wanawake wa bunge hilo.
Aidha wabunge wanawake hao wamejivunia mafaniko ya wanawake wa Ukanda huo wa kuweza kuwa na Rais,Samia Suhulu Hassan na maspika wa tatu katika mabunge sita ya nchi wanachama.
Katibu Mkuu wa Umoja wa wanawake wa EALA, Fatma Ndayigiza amewaeleza waandishi wa habari muda mfupi baada ya bunge hilo kupitisha muswada huo.
“Tumesimama hapa kama wabunge wanawake wa EAC lakini tupo na wabunge wanaume wako na sisi bega kwa bega lakini tuna vijana wadogo hapa (wanafunzi) wamesimama na sisi hawa ndiyo Taifa la kesho,” amesema Ndangiza na kuongeza.
..Kesho watakuwa wamemaliza shule na watakuja kukaa pale tulipokaa. Kauli mbiu inasema ‘Usawa wa leo ni usawa wa kudumu wa kesho’ hapa tunaongelea maendeleo ya wanawake katika muktadha wa kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili wanawake wa EAC kwa kuwahusisha vijana kesho jambo litakalotuhakikishia kuwa tumepatia tatizo hilo suluhisho la kudumu.
..Tumepitisha muswada kwenye bunge wa kutambua rasmi Umoja wa Wanawake wa EALA japo kuna changamoto lakini tunajivunia tumepiga hatua kubwa sana ambapo tuna mwanamke ambaye ni Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan tunajivunia kwa bara zima la Afrika, EAC ndiyo tuna Rais mwanawake aliyepo madarakani,”.
Ndangiza amesema pia ukanda wa EAC kuna maspika wanawake nchini Tanzania, Rwanda na Sudani ya Kusini na mawaziri wanawake wengi kwenye serikali za nchi zinazounda EAC ambapo wanafikia zaidi ya asilimia 30, ila Rwanda wanafikia asilimia 63 huku akifafanua kuwa licha ya kuwa bado kuna changamoto lakini wanafurahia mafaniko hayo.
“Tunaadhimisha siku ya wanawake tunafurahia mafanikio hayo lakini tunazikumbusha nchi wanachama ili waweze kutatua changamoto zilizobaki,” anasisitiza balozi Ndangiza ambaye ni mbunge wa EALA kutoka Rwanda.
Alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana wa kike kuwa ni pamoja na kunyimwa fursa ya kupata elimu ambapo wakati vijana wa kiume wakiwa shule wao wanakuwa nyumbani wakihudumia familia na ilijitokeza zaidi wakati wa janga la UVIKO 19 ambapo watoto wengi wa kike walishindwa kuendelea na shule .
“Wazazi watoe kipaumbele watoto wa kike kupata elimu kwani ndiyo ufunguo wa maendeleo utakaomuwezesha kuwa kiongozi wa kesho,” anasisitiza balozi, Ndangiza
Mimi nimefurahi kufika hapa EAC nimejifunza mambo mengi kuhusu haki za wanawake na tumefurahi kusikia na sisi tunaweza,” amesema Debora Walid mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Peace House iliyopo jijini Arusha.
Mwanafunzi mwingine Nancy Paul amesema kuwa alifurahi kusikia kuwa wanawake wanaweza na wamefanikiwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi mpaka ngazi ya Urais.
Umoja wa wanawake wa EALA unalenga kuhamasiha mtangamano wa jumuiya ulio imara kwa kushirikiana na wanaume kuona namna ya kuwaleta wanawake wengi kwenye nafasi za maamuzi
Mkataba wa kuanzishwa EAC kipengele cha 121 na 122 kimeelekeza kuanzishwa kwa umoja huo ambapo nchi za EAC zimeonyesha kwa vitendo namna wanathamini na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya ukanda wa EAC.
Home
Unlabelled
EALA WAPITISHA MUSWADA WA UMOJA WA WANAWAKE WENYEWE WASEMA MAZITO
Post A Comment: