Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewapongeza wakazi wa Kijiji cha Lemoot kilichopo Kata ya Lemooti Wilaya ya Monduli kwa kuchanga fedha Shilingi Milioni 125 na kufanikisha kujenga jengo la kutolea huduma za afya.
Dkt Mollel ametoa pongezi hizo leo mara baada ya kutembelea kijiji hicho na kufurahishwa na namna wananchi walivyojitokeza kuchangia kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndani ya Kijiji chao.
"Ni kitu cha ajabu mno wananchi kuchangia milioni 125, hongera kwa viongozi kwa kuhamasisha na wananchi kuchangia kwa ajili ya maendeleo yenu wenyewe" amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuhakikisha inaleta fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo na nyumba ya mtumishi pamoja na kusogeza huduma karibu zaidi kwa wakazi wa Lemooti.
"Nimeambiwa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli imeleta Milioni 20, Serikali kuu 40, mimi nnaahidi nitaenda kupambana ili kukamilisha majengo yote muhimu na huduma itolewe kwa ufanisi" amesema Dkt. Mollel
Aidha Dkt. Mollel amewataka wakazi wa Kijiji cha Lemoot kutoharakisha kukimbilia usajili wa Kituo cha Afya badala yake waanze taratibu kwa kutoa huduma za Zahanati huku akisisitiza huduma za mama na mtoto kuanza kutolewa mapema.
Awali akizungumza, Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Frank Mwaisumbe amewapongeza wakazi wa Lemoot kwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kutolea huduma za afya pamoja kuwa na usimamizi imara wa kuhakikisha kuwa jengo linakamilika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli Mhe Izack Copriano amesema kuwa Halmauri yake itaendelea kuhakikisha Wakazi wa Lemoot na Monduli kwa ujumla wanapata huduma bora za kijamii karibu na makazi yao
"Tunawapongeza wana Lemoot kwa kuchanga Milioni 125 sisi Halmashuri tulichanga Milioni 20 na hapa tumetoka kupitisha fedha nyingine Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa nyumba ya watumishi" amesema Mhe. Copriano.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mhe. Isaya Lembekule amesema kuwa kukamilika na kuanza kutolewa huduma katika majengo hayo itakuwa ni furaha kubwa kwa wakazi wa Lemoot kwakuwa wamekuwa wakisafiri umbali wa zaidi ya Kilomita 70 kufuata huduma za afya.
Post A Comment: