Na Fredy mgunda,Iringa.
MKUU wa wilaya ya Iringa
Mohamed Hassan Moyo ameutaka uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa
za Idodi na Pawaga (Mbomipa) kuacha mara moja kutumia
madaraka yao vibaya na kuwa chanzo cha migogoro baina ya jumuiya hiyo na
wawekezaji.
Akizungumza wakati mafunzo kwa
viongozi na wadau wa jumuiya hiyo,Moyo aliwataka viongozi hao kutafakari zababu
zilizopelekea kufutwa kwa MBOMIPA miaka mitano iiliyopita na kuzifanyia kazi
ili kuwa funzo la kukomesha migororo katika awamu hii.
Kiongozi huyo wa Wilaya ya
Iringa alisema Serikali haiko tayari kushuhudia viongozi wa MBOMIPA wakitumia
madaraka yao vibaya kwa kukwamisha mipango na maendeleo ya jumuiya hiyo wenye
lengo la kuvutia wawezekezaji wengi zaidi katika maeneo ya hifadhi kwa manufaa
ya wananchi wa vijiji 21.
Moyo alisema Serikali ya Wilaya
ya Iringa inapenda kuona mabadiliko ya haraka katika kuimarisha uhai wa Jumuiya
ya MBOMIPA, na Ufanisi chanya wa watendaji wa kila siku huku akihimiza
ushirikiano baina ya wananchi wa vijiji vinavyonufaika, viongozi wa MBOMIPA na
serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Alisema mafunzo wanayopatiwa
viongozi na wadau wa Jumuiya hiyo ni mwanzo mzuri wa safari ya kuimarisha
MBOMIPA mpya Kwani Wanahitajika wadau wa uhifadhi ndani na nje ya nchi ili kuwezesha utaalam na
Rasirimali fedha zitakazosaidia kuinua maendeleo ya wananchi.
Aidha Mkuu wa Wilaya Mohamed
Hassan Moyo amewahimiza wadau wa Uhifadhi wa wanyama na Mazingira kuongeza jitihada
za uhifadhi wa mazingira, misitu na vyanzo vya maji ambavyo utegemewa na watu,
mifugo na wanyamapori hatua ambayo itasaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya
hali ya hewa na Tabia nchi.
“Tayari tumeanza kupata madhara
makubwa katika maisha ya binaadam na pia kwa uchumi wa wananchi wetu na kuleta
mzigo mzito kwa Taifa letu la Tanzania, Utafiti wa mabadiliko ya hali ya hewa
na Tabia nchi umebaini ongezeko la hali ya joto pia ongezeko la tofauti la
mienendo ya mvua na hasa upungufu wa rasilimali maji” Alisema Moyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa
Jumuiya ya Jumuiya
ya Hifadhi ya Wanyamapori katika Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) Jonas
Mkusa alisema kuwa kusimama kwa shughuli za Jumuia hiyo kulikuwa na athari
katika vijiji hasa kutokana na kukosa mapato yaliyokuwa yakipatikana awali
kutokana na wadau walikuwa wamewekeza katika maeneo hayo
Mkusa alisema kurejea kwa jumuia hiyo ni jambo
la faraja kwa wananchi wa vijiji 21 vinavyonufaika na MBOMIPA na kuhimiza
ushirikiano utakaosaidia kuvutia wawekezaji na kuepuka kuzalisha migogoro isiyo
na tija inayoweza kukwamisha maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Mwenyekiti aliwahakikishia wananchi na wadau
kuwa atahakikisha fursa zote zilizopo kupitia MBOMIPA zitakuwa wazi kwa ajili
ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa uongozi wa Jumuiya
hiyo hautokuwa kikwazo katika kufikia malengo.
Mbomipa ni Jumuiya
inayoshughulika na uhifadhi wa Maeneo ya hifadhi ya wanyamapori ya jamii (WMA)
nje ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Wilayani Iringa, Wanyama walioko
katika eneo hilo wanatoka ndani ya hifadhi hiyo na hifadhi ya mikumi.
Vijiji vinavyounda Jumuiya hiyo
ni Idodi, Ilolompya, Isele, Kinyika, Kisanga,Luganga, Mafuluto,Magozi,Mahuninga,
Makifu, Mboliboli, Mkombilenga, Nyamahana, Itunundu, Kimande, Malizanga,
Mbuyuni, Mapogolo, Kitisi na magombwe.
Post A Comment: