Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Dkt. Selemani Jafo, akizungumza na vijana wa vyuo mbalimbali vya Mkoa wa Dar es Salaam (hawapo pichani) katika mkutano wa elimu ya mazingira ulioandaliwa na Global Youth Parliament, uliofanyika katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekinolojia Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa Mkutano wa elimu ya Mazingira kutoka vyuo vikuu vya Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo, akiwa meza kuu wakati wa Mkutano wa elimu ya mazingira, iliyoandaliwa na Global Youth Parliament uliyofanyika Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.
*********************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema kuwa ajenda ya Mazingira ni ya kila mtu, kwani hali ya joto imeongezeka kwa kasi na kupelekea ukame ambao Taifa letu limeshuhudia maeneo mbalimbali maji yalikuwa hayapatikani, na Jiji la Dar es Salaam lilipata mgao mkubwa wa maji pamoja na umeme hii ni kutokana na uharibifu wa mazingira.
Aliyasema hayo alipokuwa katika mkutano wa utoaji elimu kwa vijana ulioandaliwa na Global Youth Parliament uliofanyika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekinolojia (COSTECH) uliopo Kijitonyama, Jijini Dar es Salaam. Mhe. Jafo amesema kuwa uchafuzi wa mazingira unaweza kuathiri uchumi wa Nchi akatolea mfano kipindi cha kati ya mwezi wa saba mpaka wa kumi na mbili Nchini, kulikuwa na ukame wa hali ya juu na kusababisha baadhi ya viwanda kushindwa kuzalisha kutokana na mgao wa umeme uliojitokeza.
Aidha ameongeza kuwa, ajenda ya mazingira ni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivyo ni vizuri kumuunga mkono ili kuweza kufikia adhima hiyo.
"Mnamo tarehe 5/6/2021 tuliweza kuzindua kampeni kabambe iitwayo “Mazingira yangu, Tanzania yangu Ninaipenda Daima” kampeni hiyo ina chembechembe za kizalendo yenye ajenda ya kwamba sasa mazingira tuyabadilishe iwe ni suala zima la maisha yetu. Kila mtu alibebe suala la mazingira kama suala lake binafsi na ndio maana hivi juzi tumezindua kampeni iitwayo soma na mti hii ni sehemu ya kampeni kabambe ya Mazingira yangu, Tanzania yangu Ninaipenda Daima ni kwamba Nchi yetu ina wanafunzi takribani million 14.1 wa shule ya msingi na Sekondari ndio maana tukasema kila mwanafunzi apande angalau mti mmoja.”
Kwa upande wake Bw. Arnold Mapinduzi Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC), amesema kuwa moja ya jukumu la NEMC ni kutoa elimu ya mazingira Kwa jamii hivyo kuwepo kwa vijana kama hawa ni fursa kwa NEMC na Taifa kwa ujumla, kueneza elimu kwa vijana ni nyenzo kubwa katika kufikisha ujumbe kwa jamii Kwa hiyo wanapokuwa na jambo hili mapema watasaidia kuelimisha ndugu,wazazi hata vijana wenzao.
Vile vile Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekinolojia (COSTEC) Dkt. Philbert amewapongeza vijana hao kwa juhudi wanayoifanya katika kutoa elimu kwa vijana wenzao juu ya masuala mazima ya mazingira.
Post A Comment: