Induction 6: Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji George Lugome akiwasilisha mada mada juu ya majukumu ya idara yake kwa watumishi waliohamia katika utumishi wa umma kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)Afisa Sheria Mwandamizi Janet Mugini mwenye Komputa mpakato akiwasilisha mada juu ya majukumu ya Kitengo cha Huduma za Sheria kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo amewataka watumishi waliohamia katika mamlaka hiyo kutoka halmashauri, wizara na taasisi nyingine za serikali kutekeleza majukumu yao kwa weledi huku wakizingatia maadili ya utumishi wa umma.
Dkt. Ngailo ametoa wito huo tarehe 09 Februari, 2022 alipokuwa akifungua mafunzo kwa watumishi hao yaliyolenga kuwapatia uelewa wa majukumu yanayotekelezwa na TFRA ili kuwarahisishia watakapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akiyataja maadili hayo, Dkt. Ngailo amesema ni pamoja na uaminifu, utunzaji wa siri za ofisi, kutojihusisha na ulevi hasa wakati wa kazi, kujituma katika kazi, kuepuka kujihusisha na masuala ya rushwa.
Akisisitiza kuhusu rushwa, Dkt. Ngailo amesema rushwa ni adui wa haki na inaathiri sana utendaji wa kazi kwa mtoaji na mpokeaji wa rushwa na kuwahakikishia watumishi hao kuwa yeyote atakayejihusisha ya aina yoyote ile hatavumiliwa na hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria za utumishi wa umma. Hivyo, ni muhimu kuzingatia utekelezaji wa majukumu kwa ueledi na si vinginevyo.
Akizungumzia suala la ulevi, Dkt. Ngailo amewataka watumishi hao kujiepusha na masuala ya unywaji wa pombe na ulevi hasa wakati wa kazi na kwamba kujihusisha na jambo hilo kutawafanya kutokidhi vigezo vya kutumika katika mamlaka na serikali kwa ujumla.
Aidha, Dkt.Ngailo amewataka watumishi waliopangwa kutekeleza majukumu yao katika ofisi za kanda kuhakikisha wanaimarisha mahusiano baina ya ofisi zao (TFRA - kanda) na halmashauri pamoja na wadau wengine wa mbolea hapa nchini.
Pamoja na hayo amewataka watumishi hao kuwa mawakili wazuri katika kutumia rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na magari na samani zinazotumika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Ili kufanukisha hili, ushirikiano na mipango mizuri katika utekelezaji wa majukumu utasaidia katika kuhakikisha rasilimali za serikali zinatumika kwa ufanisi na thamani ya fedha itaonekana. Dkt. Ngailo alisisitiza.
Akizungumzia majukumu ya TFRA; Dkt. Ngailo alisema ni pamoja na udhibiti wa ubora wa mbolea, uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima kwa kushirikiana na halmashauri na wadau mbalimbali, kutoa ushauri kwa serikali kuhusu masuala yanayohusiana na mbolea, kushirikiana na wadau wengine katika masuala yanayohusiana na mbolea na kushirikiana na taasisi nyingine za serikali katika kuhakikisha mbolea bora inawafikia wakulima kwa wakati.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mada; Kaimu Mkurugenzi wa huduma za udhibiti Bw. Gerod Nganilevanu alisema awali udhibiti wa mbolea ulikuwa ukisimamiwa na Shirika la viwango nchini (TBS). Hata hivyo, kutokana na majukumu mengi ya TBS na mahitaji makubwa ya wakulima na wadau wengine kuhusiana na mbolea, Serikali iliona ni vema kuanzisha mamlaka itakayosimamia na kuhakikisha inarahisisha upatikanaji wa mbolea inayokidhi viwango na kwa wakati.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Pamoja Stevenson Ngoda alisema idara yake ina jukumu la kuratibu masuala ya ununuzi wa pamoja wa mbolea na kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa mbolea ili kuwapunguzia wakulima mzigo wa kununua mbolea zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa.
Wakati huohuo akiwasilisha mada kwa niaba ya Meneja wa Huduma za Sheria, Afisa Mwandamizi wa Sheria Bi. Janet Mugini amesema kitengo cha huduma za sheria kinajihusisha kutoa huduma na ushauri wa kisheria na kuhakikisha mamlaka inaendeshwa kwa mujibu wa sheria kama ilivyokusudiwa
Kwa upande wake, Afisa Tehama Salehe Kejo amewapitisha watumishi hao kwenye mfumo unaotumiwa na mamlaka hiyo katika masuala ya usajili wa wafanyabiashara, wazalishaji na wasambazaji wa mbolea nchini. Zaidi, amesema jukumu kubwa la kitengo cha tehama ni kusimamia mifumo yote ya tehama inayotumika katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya mamlaka hiyo
Mwisho Kaimu Meneja wa idara ya Mipango na Upelemaji Bw. George Lugome amesema lengo kuu la TFRA ni kuhakikisha mbolea inayokidhi viwango inawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei wanayoweza kuimudu. Hata hivyo, amesema kutokana na mbolea kupanda kwenye soko la dunia kwa mwaka huu; hali hiyo imeathiri soko la mbolea nchini. Mamlaka na Serikali kwa ujumla inaifanyia kazi changamoto hii ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa msimu huu wa kilimo.
Naye Meneja wa Kitengo cha Manunuzi, Joseph Hilary amewataka watumishi hao kuzingatia taratibu za manunuzi wakati wote wa utumishi wao ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.
Mafunzo hayo ni kwa mujibu wa miongozo ya utendaji wa Mamlaka yanayofanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 9 hadi 11 Februari, 2022.
Post A Comment: