Na. Angela Msimbira MARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Innocent Bashungwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi walizozifanya wakurugenzi wote wa Halmashauri katika kipindi cha miezi sita ili kuweza kufanya tathmini ya utendaji kazi wao.
Akihutubia wananchi wa Mkoa wa Mara leo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu J.K Nyerere, iliyojengwa katika Kata ya Kwangwa, Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Mhe. Samia amesema wakurugenzi hao walikuwa kwenye kipindi cha uangalizi wa miezi sita hivyo ni wajibu wa Serikali kuwafanyia tathmini utendaji kazi wao.
“Wakurugenzi mlikuwa katika kipindi cha matazamio miezi sita tangu mlipoteuliwa mpaka mtakapofika februari 18, 2022 ninamuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI kuniletea taarifa ya kina kuhusu utendaji kazi wa kila Mkurugenzi nchini kwa kuangalia kazi walizozifanya” amesisitiza Mhe. Samia
Amesema taarifa hiyo itasaidia kujua Wakurugenzi waliofanya vizuri katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi wanatakiwa kubaki kuendelea na majukumu yao na wanaopaswa kuondolewa.
Kuhusu ubadhilifu wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoa wa Mara Mhe. Samia amesema, kumekuwepo na ufujaji mkubwa wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uchelewashwaji wa miradi hiyo hali inayopelekea kurudisha nyuma maendeleo Mkoani hapo.
Mhe. Samia ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Mara kujitathmini katika suala zima la usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuhusu Wakuu wa Idara amesema, kuna baadhi ya Wakuu wa Idara watatakiwa kuondolewa kutokana na kufanya kazi kwa mazoea.
Aidha, ameagiza kutumika kwa kamati za usimamizi zilizotumika katika ujenzi wa madarasa kwenye utekelezaji wa miradi inayoendelea ya ujenzi wa vituo vya afya na miradi ya maji nchini.
Aidha, amesema kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo nchini lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaenda kutekeleza miradi inayotatua kero za wananchi nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi amesema,8 kumekuwa na changamoto kubwa kwa Wakuu wa Idara kwa kuwa baadhi yao ni wabadhilifu wa fedha za Serikali na kufanyakazi kwa mazoea.
Post A Comment: