Uongozi wa Pori la Akiba la Pande, lililo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), umepanda miti 300 katika shule za msingi Kibese na Mabwepande, mkoani Dar es Salaam, lengo likiwa ni kupanda miti 250,000 katika maeneo yote jirani na pori hilo.


Akizungumza na wanahabari kuhusu utaratibu huo, Meneja wa pori hilo Honest Buretta, amesema uamuzi huo una dhamira ya kulifanya Pori la Pande lisionekane kama kisiwa.

"Tutapanda miti katika shule za msingi, sekondari, mashamba na makazi ya watu walio jirani nasi, lengo likiwa ni kulifanya pori letu la Pande lisionekane kama kisiwa cha msitu, bali misitu ionekane kuanzia kwenye makazi ya watu," amesema.

Honest ameongeza kuwa, ili kutekeleza azma hiyo, wanashirikiana na wadau mbalimbali, zikiwemo serikali za mitaa, kampuni binafsi rafiki wa mazingira, shule za sekondari, msingi na wananchi kwa ujumla.

Amesema kwa shule, wametumia klabu za mazingira kufikisha elimu ya umuhimu wa upandaji miti, ili kuhamasisha jamii kutunza mazingira na uhifadhi wa maliasili za taifa la Tanzania.

Akizungumzia ushirikiano uliopo baina ya Pori la Pande na jamii, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mabwepande, Mwalimu Mangwala, amesema tangu TAWA ilipokabidhiwa pori hilo ushirikiano uneongezeka kati ya wananchi na wahifadhi.

Mangwala amesema, ushirikiano huo umekwenda mbali zaidi mpaka kwenye masuala ya kijamii, ambayo kwa utaratibu maalumu, jamii za jirani hupata msaada kutoka TAWA ikiwemo ajira za muda mfupi kwa vijana.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibese, Nestor Masunga, amesema uwepo wa Pori la Pande katika eneo lao, umekuwa jambo jema kwao kutokana na mengi mazuri ambayo jamii ya shule inajifunza hususan umuhimu wa utunzaji wa mazingira.

Mwenyekiti wa Klabu ya Mazingira katika Shule ya Msingi Mabwepande, Caroline Joseph, amesema miti inayopandwa na TAWA shuleni hapo, ina manufaa makubwa ya kulinda mazingira yanayotumiwa na wanafunzi hao kujisomea.

Mwanafunzi huyo wa darasa la sita ameahidi kuwa, wataitunza miti hiyo muda wote watakapokuwa shuleni hapo, ili iwanufaishe wanafunzi wengine na jamii za jirani baada ya wao kuhitimu.

Share To:

Post A Comment: