**********************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na operesheni, Misako na doria mbalimbali za magari, pikipiki, miguu na Mbwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kuzuia, kudhibiti na kupambana na uhalifu wa aina zote. Katika Misako iliyofanyika kuanzia tarehe 07/02/2022 hadi tarehe 10.02.2022 watuhumiwa mbalimbali wa makosa ya mauaji, kusafirisha madini bila kibali, kupatikana na dawa za kulevya, kupatikana na pombe haramu ya Moshi wamekamatwa kama ifuatavyo:-
KUTOROSHA MADINI NJE YA NCHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa Madini Wilaya ya Chunya limefanikiwa kukamata madini aina ya dhahabu yenye thamani zaidi ya Tshs.milioni mia arobaini.
Ni kwamba mnamo tarehe 09.02.2022 majira ya saa 19:30 usiku huko katika kizuizi cha Polisi Chalangwa kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi kwa kushirikiana na Maafisa Madini Wilaya ya Chunya walikamata Gari T.948 DTM aina ya Toyota Crown iliyokuwa ikiendeshwa na mtu aliyefahamika kwa jina BARAKA SINGU @ NYODA, ambaye baada ya kusimamishwa kwenye kizuizi hicho alikimbia na kutelekeza gari hiyo.
Katika upekuzi uliofanywa kwenye Gari hiyo vilikutwa vipande 36 vya madini aina ya dhahabu vyenye uzito wa gramu 1367.07 vyenye thamani ya Tshs. 147,694,961.83/= na fedha taslimu Tshs. 504,600/=. Lengo ni kukwepa kodi na tozo za serikali. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa kwa hatua zaidi za kisheria. Aidha linatoa rai kwa wafanyabiashara kutambua kuwa mkono wa serikali ni mrefu hivyo ni vyema kufanya biashara halali kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo ili kuepuka kukinzana na sheria.
KUSAFIRISHA MADINI BILA KIBALI.
Katika mazingira mengine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia FELIX ULIMWENGU [42] Mfanyabiashara na Mkazi wa Madale Jijini Dar es Salaam kwa kosa la kusafirisha madini bila ya kuwa na kibali.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.02.2022 majira ya saa 14:45 mchana huko kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe kilichopo Wilaya na Mkoa wa Mbeya. wakati wa ukaguzi wa abiria waliokuwa wanasafiri kwa ndege ya kampuni ya ATCL kuelekea Dar es Salaam na kukutwa na madini aina ya Dhahabu kwenye Wallet yake yenye uzito wa Gramu 36 yenye thamani zaidi ya Tshs.Milioni nne bila kuwa na kibali.
KUPATIKANA NA MADAWA YA KULEVYA YADHANIWAYO KUWA NI HEROIN.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia LUSEKELO ELISHA MWAKANGATA [19] Mkazi wa Mama John kwa kosa la kupatikana na kete sita sawa na gramu 0.3 za madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni heroin.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 10.02.2022 majira ya saa 02:15 usiku huko maeneo ya Mama John, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya katika Misako inayoendelea maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kujihusisha na uuzaji wa dawa hizo za kulevya.
KUINGIA NCHINI BILA KIBALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia SIPO BANDA [20] raia wa nchini Malawi kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 09.02.2022 majira ya saa 00:40 usiku katika misako iliyofanyika huko Stand ya Usangu, Kata ya Itezi, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Mtuhumiwa amehojiwa na kudai kuwa alifika nchini kwa lengo la kutafuta kazi.
KUINGIA NCHINI BILA KIBALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia wahamiaji haramu kumi na moja [11] raia wa nchini Rwanda na Burundi kwa kosa la kuingia nchini bila kuwa na kibali.
Wahamiaji hao walikamatwa mnamo tarehe 07.02.2022 majira ya saa 18:00 jioni huko katika kizuizi cha Polisi Chalangwa kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya wakiwa wanasafiri ndani ya Gari yenye namba za usajili T.295 DBQ Basi mali ya kampuni ya Prince Ahmed wakitokea Tabora kuelekea Mbeya.
Wahamiaji hao wakiwemo watoto wadogo sita [06] wafahamika kwa majina:-
- AKULIMANA EMANUEL [40]
- QUIZERA RACHEL [32]
- AMANI HORESI [32],
- TUYIZERE WELLORL [32]
- MOSES RAPHAEL [20]
- KWIZELA WILES, mwaka 1.5
- BUMTUBWIMINO JEHOVANIS [14]
- MIYOBYOSE JUSTIN [06]
- ISHIMWE ALINE [15]
- SHIMI ARENI [15]
- WIZEMANA CRIMANTINE [15]
Watuhumiwa wanafanyiwa mahojiano na kisha watakabidhiwa idara ya uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria.
KUKAMATWA WATUHUMIWA WA WIZI WA PIKIPIKI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na Misako na doria dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali yakiwemo ya wizi na utapeli. Katika Misako iliyofanyika tarehe 08.02.2022 majira ya saa 01:30 usiku huko eneo la Mbalizi kati, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili [02] wa matukio ya kuvunja nyumba usiku na kuiba pamoja na matukio ya wizi wa Pikipiki.
Watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na matukio hayo ni 1. EMILY MASOUD [30] Mkazi wa Mtaa wa Relini na 2. HASSAN SIMKONDYA [42] fundi ujenzi, Mkazi wa Mapeleke. Watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kuhusika na matukio ya wizi wa Pikipiki mbili aina ya T-better na Kinglion sehemu mbili tofauti huku wakieleza mbinu wanayotumia kuiba pikipiki hizo ni kuvunja nyumba, kuiba na kuanza kukokota pikipiki hiyo na kisha kukata waya kwa ajili ya kuiwasha. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako wa kuwatafuta wanunuzi wa Pikipiki hizo pamoja na mtandao wa wizi wa Pikipiki.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ALINANUSWE KEMWA [53] Mkazi wa Ituha Jijini Mbeya kwa kosa la kupatikana na Pombe Haramu ya Moshi [Gongo] ujazo wa lita tatu [03].
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.02.2022 majira ya saa 11:00 asubuhi huko Ituha, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya katika misako inayoendelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia STEVEN KASEBWA [56] Mkazi wa Shewa Jijini Mbeya kwa kosa la kupatikana na Pombe Haramu ya Moshi [Gongo] ujazo wa lita nne [04].
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.02.2022 majira ya saa 11:00 asubuhi huko Ituha, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, katika misako inayoendelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa Pombe hiyo.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. HAWA MATOLA [36] Mkazi wa Isyesye na 2. ANYOSISYE JACKSON [40] Mkazi wa vingunguti wakiwa na Pombe Moshi kiasi cha lita nne [04].
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 09.02.2022 majira ya saa 20:30 usiku huko maeneo ya Isyesye vilabuni, Kata ya Isyesye, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya katika Misako inayofanywa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ya kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu wa matukio mbalimbali.
Post A Comment: