Na. Elinipa Lupembe.

Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha  huduma za afya nchini, huku halmashauri ya Arusha ikiwa ni miongoni mwake, kwa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hasa maeneo ya vijijini, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo za afya sambamba na  kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Katika kutimiza adhma hiyo, serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 490 kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya Mwandeti,  ili kuipa hadhi ya kuwa Kituo cha afya, kiweze kutoa huduma nyingi  zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali ikiwa ni zahanati.

Akizungumza na mwandishi wetu, mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amebainisha kuwa, halmashauri imepokea kiasi hicho cha fedha, kwa awamu tatu tofauti, kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu katika  zahanati ya Mwandeti ili kikipandisha hadhi na kuwa Kituo cha Afya.

Ametaja mchanganuo wa shilingi milioni 490, kimetumika kujenga miundo mbinu ya majengo,  ikiwa ni pamoja na jengo la mama na mtoto 'maternity ward' na jengo la upasuaji 'theater', kwa shilingi milioni 150, milioni 259 zinajenga jengo la Wagonjwa wa nje ' OPD', Maabara na kichomea taka, huku milioni 90 zikitumika kujenga nyumba moja ya watumishi yenye uwezo wa kuishi familia tatu (3 in 1).

"Nipongeze serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka na kuwahurumia kina mama wajawazito na watoto, waliokuwa wanahatarisha maisha na wengine kupoteza maisha wakati wa kujifungua, kutokana na kukosa huduma za haraka wakati wa kujifungua, uwepo wa Kituo cha afya Mwandeti kutapunguza ama kuondoa kabisa vifo visivyo vya lazima" amesisitiza Mkurugenzi Msumi.

Aidha Msumi ametaja mchanganguo wa fedha hizo, shilingi milioni 490, kulingana na vyanzo vyake kuwa shilingi milioni 240 kutoka serikali Kuu, lakini shilingi milioni 250 fedha kutoka serikali Kuu, kupitia tozo ya miamala ya simu, tozo ambazo watumiaji wote wa simu nchini wanachangia maendeleo ya nchi yao, ikiwemo wananchi wakazi wa Mwandeti. 

Naye Mganga Mfawidhi, Zahanati ya Mwandeti, Dkt. Aidan Martin, amesema kuwa, uwepo wa kituo cha afya Mwandeti, utasaidia upatikanaji wa huduma muhimu ambazo hapo awali, zilikuwa hazipatikani kwenye zahanati, huku wagonjwa wakilazimika kwenda hosptiali ya wilaya ya Olturumeti umbali wa zaidi ya Kilomita 35, jambo lililoongeza gharama na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

"Tulikuwa tunatoa rufaa nyingi kwa wagonjwa, lakini uwepo wa kituo cha afya, tunatarajia huduma nyingi zitapatikana hapa na kutakuwa na oingezeko la wagonjwa kutoka wastani wa wagonjwa 1,200 mpaka 1,700 kwa mwezi" ameweka wazi Daktari Aidan.

Hata hivyo wananchi wa kata ya Mwandeti husasani kijiji cha Engalaoni, ambao hutumia zahanati Mwandeti kwa matibabu, wameishukuru serikali kwa kuona umuhimu na kuwapa fedha za kuongeza miundo mbinu ya majengo, ili zahanati hiyo ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya jambo ambalo wamethibitisha kuwa Mungu amewaonekania kwa kusikia kilio chao.

Diwani wa kata ya Mwandeti, Mhe. Logolie Lukumay amethibitisha kuwepo kwa changamoto zakupata matibabu kwa wagonjwa wa kijiji cha Engalaoni, hasa kwa kuzingatia kijiji hicho ni cha mwisho wa kata na wilaya pia.

Amesema kuwa, kiwepo kwa Kituo cha afya, licha ya wananchi kuwa na uhakika wa kupata matibabu kituoni hapo, lakini pia kitapunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kupata matibabu kwenye hospitali kubwa na zaidi, kitasaidia kupunguza vifo visivyo vya lazima hasa kwa kina mama wajawazito wanaohitaji kufanyiwa upasuaji pamoja  na watoto  wanazozaliwa.

."Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita, tunamshukuru sana mama Samia Suluhu, ametufuta machozi ya muda mrefu, zahanati hii inahudumia watu wa Engalaoni na kata jirani ya Monduli, lakini watu waliteseka sana kupata matibabu, kina mama wajawazito wanapohitajika kufanyiwa 'operation' ilikiwa ni shida sana, usafiri nao ilikuwa  shida na umbali pia wa kufika hospitali ya wilaya ilikuwa ni tatizo" amefafanua Mheshimiwa Logolie.

Kukamilika kwa ujenzi wa miundo mbinu ya zahanati ya Mwandeti, kunategemea kukipandisha hadhi na kuwa kituo cha afya, kituo ambacho kitahudumiza zaidi ya watu elfu 15 wa kata ya Mwandeti na kata ya jirani ya Mferejini, wilaya ya Monduli.


Share To:

Post A Comment: