******************
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Serikali katika kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii katika mkoa wa Morogoro, ilipandisha hadhi sehemu ya Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa Nyerere na Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya Wami Mbiki kuwa Pori la Akiba.
Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Norah Waziri Mzeru, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa moja ya Kitovu cha Utalii duniani.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali kupitia Mradi wa Kukuza Maliasili na Kuendeleza Utalii (REGROW), inajenga barabara zenye urefu wa takribani kilometa 996, njia za watembea kwa miguu kilometa 132.5, viwanja vya ndege saba (7), malango ya kuingilia wageni nane (8), vituo vya askari nane (8), na vituo vya kutolea taarifa kwa wageni vitatu (3) katika Hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa na Nyerere mkoani Morogoro lengo ikiwa ni kukuza utalii katika mkoa huo.
Vilevile, kukamilika kwa Reli ya mwendokasi (SGR) pamoja na kutumika kwa Reli ya TAZARA kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika mikoa ya Morogoro na Pwani.
Post A Comment: