*****************

Na. John Mapepele

Maelekezo ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ya kutaka mchakato wa mwaka huu wa utoaji wa Tuzo za Muziki bila upendeleo yamefika mahali pazuri.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Matiko Mniko, leo Februari 21, 2022 imeeleza kuwa jumla ya kazi 402 zimewasilishwa kuanzia Februari 9, 2022 baada ya zoezi la kuwaelimisha wadau kukamilika na kuwa BASATA limeamua kuongeza muda wa siku saba ili kutoa nafasi kwa wasanii wengi kushiriki.

“Tunaongeza siku 7 kwa ajili ya wasanii kuwasilisha kazi katika vipengele vya Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2021)” imefafanua taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo imefafanua kwamba mwisho wa kuwasilisha kazi hizo ni Machi mosi mwaka huu kupitia link www. tanzaniamusicawards.info

Akizungumza kwenye Hafla ya Uzinduzi wa Utoaji wa Tuzo za Muziki na Ugawaji wa Mirahaba kwa Wasanii Januari 28, 2022 kwenye Ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere. Mhe, Mchengerwa alilielekeza (BASATA) kutenda haki ili kupata kazi zenye kiwango bora.

Aidha, alilielekeza kutoa muda wa kutosha kwa wasanii wa kuwaelimisha wasanii kuhusu tuzo hizo na kutoa muda wa kutosha wa kuwasilisha kazi zao.

Alilitaka kufanya kazi yake ya kukuza, kuendeleza na kuwasaidia wasanii wa Tanzania kwa weledi na kuacha mara moja kufanya kazi kwa mazoea, na kusisitiza waanze kufikiria kuandaa tuzo kubwa za kimataifa.

"Natambua huko nyuma kumekuwa na malalamiko naomba niwaonye, mimi katika kipindi changu hakutakuwa na tuzo za msongo”. Alisisitiza Mhe, Mchengerwa.

Aliwashauri wasanii kujisajiri COSOTA ili kazi zao ziweze kutambulika na kunufaika nazo.

Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt. Hassan Abbasi alisema Serikali imefufua tuzo hizo baada ya miaka saba kutokuwepo hivyo wadau wa sanaa kwa kushirikiana na Serikali wana wajibu wa kuzilinda na kuzienzi ili ziendelee kuwanufaisha.

Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu alisema Sekta ya Sanaa inagusa maisha ya wananchi wote hivyo Wizara itahakikisha inaandaa mazingira bora ili wasanii wanufaike na kuboresha maisha yao.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: