NA Yeremias Ngerangera-Namtumbo
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma limemkataa afisa manunuzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa madai ya kuchelewesha manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi .
Akitoa maamuzi ya baraza hilo mwenyekiti wa baraza la madiwani halmashauri ya wilaya Namtumbo Juma Pandu alisema afisa manunuzi wa halmashauri hiyo atafute halmashauri nyingine ya kufanyia kazi na sio halmashauri ya Namtumbo.
Pandu alidai maamuzi hayo yamefikiwa na baraza hilo baada ya madiwani kukilalamikia kitengo hicho kwa muda mrefu juu ya ucheleweshaji wa ununuzi wa vifaa vya ujenzi bila kuwepo kwa mabadiliko.
Awali mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Kenneth Ningu aliwaagiza madiwani katika salamu zake za serikali katika baraza hilo kuwa wanatakiwa kuchukua maamuzi magumu katika kitengo hicho cha manunuzi kwa kuwa kimekuwa kero kwa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
“Nimefanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa vyoo katika zahanati wilaya nzima ya Namtumbo kero kubwa inaelekezwa idara ya manunuzi kuchelewesha ununuzi wa vifaa ”alisema mkuu wa wilaya.
Kwa mujibu wa afisa manunuzi Mwenyewe Samson Manjale alipohojiwa juu ya uamuzi huo akiwa ukumbini hapo alisema alitegemea kuwepo kwa maamuzi hayo kutokana na misimamo yake ya kusimamia miongozo ya serikali kwa kutowapa kazi baadhi ya waheshimiwa madiwani waliomba kujenga baadhi ya majengo katika kituo cha afya magazini , ujenzi wa majengo ya Hospitali ya wilaya na vyoo vya zahanati na kushuhudia upinzani mkali wa kutaka kumwondoa katika Halmashauri hiyo.
Manjale alidai swala la kukilalamikia kitengo cha manunuzi kuchelewesha manunuzi sio kweli kwani yeye haandiki dokezo la kuomba vifaa bali idara na wakuu wa zahanati zinazotekeleza mradi kuwahisha maombi na idara ya manunuzi itashirikiana na idara ya ujenzi kujiridhisha vifaa vinavyotakiwa kununuliwa na idara ya fedha kumlipa mzabuni kwa wakati badala ya kukilaumu kitengo cha manunuzi pekee.
Manjale alidai kwa kawaida mzabuni anatakiwa kutoa huduma ya vifaa kabla ya kulipwa fedha zake sasa katika halmashauri yetu wazabuni wanatoa huduma halafu fedha zao hawalipwi kwa wakati hivyo kitengo cha manunuzi kinapata wakati mgumu kuwaomba wazabuni kuendelea kutoa huduma wakati madai yao mengine ya nyuma hayajalipwa.
Hata hivyo Manjale alifafanua kitengo cha manunuzi tu ndicho kinacholaumiwa hata ikiwa kitengo kimemaliza hatua za manunuzi na kitengo cha fedha kinachelewesha kuwalipa wazabuni madeni yao ya nyuma ili waweze kuendelea kutoa huduma bado hoja ya lawama zinabebwa na kitengo cha manunuzi pekee alisema Manjale.
Aidha Manjale alifafanua kuwa hoja ya kumwondoa katika halmashauri hiyo ilitamkwa na waheshimiwa baada ya kuwanyima baadhi ya kazi za ujenzi walizoomba katika kituo cha afya magazini na hospitali ya wilaya alisema manjale.
Wakati afisa manunuzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo akiambiwa kutafuta Halmashauri nyingine ya kufanyia kazi ,mkuu wa idara ya afya Lucia Kafumu akipewa miezi mitatu ya matazamio juu ya mienendo isiyoridhisha ya idara yake na kupewa muda huo wa kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika idara yake .
Mkuu wa wilaya Namtumbo Dkt Julius Kenneth Ningu akitoa salamu za serikali katika mkutano wa baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya Namtumbo.
Post A Comment: