Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) leo tarehe 10 Februari, 2022 umetoa mafunzo juu ya mfumo mpya wa ukusanyaji wa ushuru wa maegesho kwa njia ya kielektroniki kwa Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara, Maafisa Tarafa pamoja na Watendaji Kata Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro.
Mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa ushuru wa maegesho unatarajia kuanza kutumika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 01 Machi, 2022 ambapo mtumiaji wa maegesho atatakiwa kulipa Shilingi 300 kwa Saa na Shilingi 1,000 kwa Siku.
Mfumo wa Maegesho Kidigitali (TeRMIS) ni mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto (parking fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges) pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara.
Mtumiaji wa maegesho atapaswa kulipia maegesho baada ya kupatiwa kumbukumbu namba ya malipo (control number) na atatumia Kumbukumbu namba hiyo kulipia maegesho kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala wa Huduma za fedha.
Mfumo huu wa Maegesho Kidigitali umetoa muda muafaka kwa mtumiaji wa maegesho kulipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya Shilingi10,000/=.
Post A Comment: