Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh Andrew Kundo, (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milisic, Mwakilishi mkazi shirika la Umoja wa Mataifa Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO Tanzania, Bw. Tirso Dos Santos na Prof. Bernadeta Killian Naibu Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dkt. Mona Mwakalinga Amidi Mkuu Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kwenye maadhimisho ya kitaifa ya Redio Duniani ndani ya Ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu cha Dar -es-Salaam.
Maadhisho ya 11 ya Siku ya Redio Duniani 2022, yamefanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu cha Dar -es-Salaam yamebeba kauli mbiu "Redio na Uaminifu".

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Andrew Kundo, akifatilia kwa umakini Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Redio Duniani katika Ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu cha Dar -es-Salaam.

 
Pichani ni Wadau mbalimbali waliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa maktaba mpya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



 Naibu Waziri wa Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh Andrew Kundo amewataka waandishi wa habari nchini kuboresha maudhui wanayoyarusha katika redio mbalimbali nchini ili kuongeza uaminifu kwa wasikilizaji kwa kurusha taarifa zilizochunguzwa kwa kina na kujenga jamii yenye maisha bora.


Akizungumza mapema hii leo wakati wa maadhimisho ya siku ya Redio duniani yaliyoandaliwa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma katika ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na UNESCO akimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Nape Nauye, Naibu Waziri amesema uaminifu kwenye uandishi wa habari za redio unategemeana na maidhui ya hali ya juu yanayotengenezwa.

"Ukuaji huu wa redio umesaidia sana kufikisha taarifa kwa urahisi kwa wananchi, tafiti mbalimbali zinaonesha vituo hivi vya redio maarufu kama redio za mikoani au redio za jamii zinasikikizwa zaidi kwenye maeneo zilizopo kutokana na ukweli kwamba zinarusha maudhui yanayogusa wananchi wa maeneo hayo, hivyo waandishi lazima waendelee kujikita kwenye taarifa ambazo zinafanyiwa uchunguzi na ambazo zitakuwa na manufaa kwa umma na zitasaidia kujenga jamii yenye maisha bora baadae" amesema.

Amesema, kutokana na maendeleo ya kidijitali kumekuwa na wimbi kubwa la kutoheshimu maadili ya uandishi wa habari kutokana na usambazaji wa taarifa zinazokosa weledi, hivyo amevitaka vituo vya habari viwe sehemu ya maisha ya wasikilizaji wao kwa kuzalisha maudhui yanayoendana na hadhira wao ili kuendeleza imani kwa wasikizaji.

Vilevile katika hotuba yake ya uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya redio duniani, Naibu Waziri wa Habari na Mawasiliano Mh Andrew Kundo, amevihakikishia vituo vya habari nchini kuvitatulia changamoto zinazovikumba kwa kushindwa kuendana na teknolojia ya sasa kufuatia viwango vya kati vya biashara, hivyo kuangalia namna ya kuviwezesha kujitegemea kifedha na kujiamini na kubaki kwenye biashara hasa katika kipindi hiki kigumu cha Uviko-19, kutokana habari, mawasiliano na TEHAMA kuwa fursa katika redio na kupelekea kuimarisha utoaji huduma zao.

Kwa upande wake Mratibu wa maadhimisho hayo Abdallah Katunzi, ameeleza kuwa siku ya redio duniani ina umuhimu mkubwa wa kukuza uelewa na umuhimu wa redio kwa jamii, kuhamasisha viongozi na watunga sera kufikisha taarifa kwa jamii na kutengeneza mshikamano kati ya taasisi za Habari ndani ya jamii husika.

Mwakilishi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania Bwn. Tirso Dos Santos amesema redio inabaki kuwa chombo muhimu sana katika maendeleo ya jamii kutokana na mchango mkubwa wa kuhabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya uwajibikaji wa viongozi, mapambano dhidi ya Uviko-19, harakati za kumuinua mwanamke na kuwapa kipaumbele watu wa makundi maalumu kujiinua kiuchumi kutokana na mijadala mbalimbali inayowekea na vyombo vya habari nchini.

Maadhimisho ya siku ya redio duniani yanafanyika kila mwaka tarehe 13 Mwezi wa 2, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya 11 yenye kauli mbiu "Redio na Uaminifu".

Share To:

Post A Comment: