Baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa) |
Fuso likishusha baadhi ya mabomba yatakayojenga miradi minne ya maji wilayani Lushoto kwa fedha za UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa)
Na Yusuph Mussa, Lushoto
Wilaya
ya Lushoto mkoani Tanga imepata fedha za UVIKO 19, ambapo miradi minne
ya Bungoi, Kwesimu, Mbwei na Mayo itatekelezwa mwaka huu ili kuwaondolea
kero ya maji wananchi.
Hayo
yalisemwa Februari 13, 2021 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa
Mazingira Mijini na Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin
Sizinga kwenye hafla fupi ya Mkuu wa Wilaya hiyo Kalisti Lazaro kupokea
mabomba yenye urefu wa kilomita 33.6 yakiwa yenye kipenyo tofauti kwa
ajili ya miradi hiyo, iliyofanyika Ofisi za RUWASA Lushoto.
"Serikali
imetupatia mabomba yenye urefu wa kilomita 33.6 kwa ajili ya
utekekezaji wa miradi minne kupitia fedha za UVIKO 19. Miradi hiyo ni
ule wa Bungoi ambao kutakuwa na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lita
175,000, ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea
maji, uchimbaji wa mtaro mita 13,500, ulazaji wa mabomba ya kusafirisha
maji mita 4,200 na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mita 9,300,
mradi wote ukigharimu sh. milioni 507.
"Ukarabati
wa chanzo cha maji Kwesimu utagharimu sh. milioni 250, ambapo kazi zake
ni ujenzi wa chanzo cha maji, ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji
mita 2,800, uunganishaji wa bomba kwenye tanki na uchimbaji wa mtaro
mita 2,800" alisema Sizinga.
Sizinga
alisema mradi mwingine ni ule wa Mbwei, ambapo kazi zake ni ujenzi wa
chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la kusafirisha maji mita 1,500,
uunganishaji wa bomba kwenye tenki, uchimbaji wa mtaro mita 8,800,
ulazaji wa bomba, ujenzi wa tanki lita 90,000 na ujenzi wa vilula (DP),
gharama yake ikiwa sh. milioni 280.
Mhandisi
Sizinga alisema mradi mwingine ni Mradi wa Maji Mayo uliopo Halmashauri
ya Bumbuli, ambao utagharimu sh. 497,960,800, na shughuli
zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la
kusafirisha maji mita 1,100, uunganishaji wa bomba kwenye tenki,
uchimbaji mtaro mita 6,800, ulazaji wa bomba na ujenzi wa tenki la
kuhifadhia maji lita 90,000.
Mkuu
wa Wilaya, Lazaro, alimshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa
kupeleka fedha za UVIKO 19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema wilaya hiyo haina shida ya vyanzo vya maji, bali miundombinu ya
maji, hivyo kwa kupeleka fedha hizo, wananchi wa Lushoto watapata maji
safi na salama.
"Tunamshukuru
Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kutuletea
fedha hizi za UVIKO 19, sasa ameonesha kuwajali wananchi wa Lushoto, na
sasa tutapata maji kwa zaidi ya asilimia 70. Sisi wananchi wa Lushoto
hatuna shida ya vyanzo vya maji, bali miundombinu yetu ya maji ndiyo
chakavu, hasa katika mji wa Lushoto. Lakini kwa baadhi ya vijijini,
miundombinu hiyo ilikuwa haijafika kabisa" alisema Lazaro.
MWISHO.
Post A Comment: