Mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Mageuzi ya Kijani Afrika(AGRA) na Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Dr.Jakaya Mrisho Kikwete amepongeza jitahada kubwa zinazofanywa na AGRA nchini Tanzania katika kukuza kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Dr Kikwete ameyasema hayo leo Mkoani Iringa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya kilimo inayofadhiliwa na AGRA ambapo amepata fursa ya kuwatembelea wachakataji wa mazao ya kilimo na wauzaji wa pembejeo na kujionea namna ambavyo wadau hao wa kilimo wamesaidia kujiongezea kipato na kutengeneza fursa nyingi za Ajira kwa wakulima wengi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya Kilimo.
“Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mipngo ya AGRA,tulikubaliana kwenye Bodi kwamba wajumbe tupite kukagua miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na AGRA.
Nimefarijika kuona miradi mingi ni mizuri na imeleta athari chanya kwa wakulima wetu na wachakataji wa mazao ya kilimo,hii itasaidia sana kukuza sekta ya kilimo na kukuza uchumi wa Nchi yetu”Alisema Dr Kikwete
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde ameishukuru AGRA kwa kazi kubwa inayofanya katika kumjengea uwezo mkulima wa nchi hii na kuhakikisha kwamba zao la kilimo linaongezewa thamani jambo ambalo ndio muelekeo wa serikali na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo ili malengo ya nchi kupitia kilimo yaweze kutimia.
Katika ziara hiyo ya siku 5 Dr Kikwete ameongozana na Makamu wa Rais wa AGRA Bi. Aggie Asimwe Konde pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo.
Post A Comment: