Sehemu ya majengo ya chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa ambacho serikali ya Awamu ya Sita imetoa shilingi Bilioni 2.035 hivi karibuni kukamilisha mradi huo uliopo mjini Sumbawanga. Ujenzi utakamilika mwezi Mei mwaka huu chini ya wakandarasi Chuo cha Ufundi Arusha.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti juzi akitoa maelekezo kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Sumbawanga juzi alipokagua kazi ya ukamilishaji mradi huo kufuatia serikali kutoa shilingi Bilioni 2 kukamilisha mradi huo .

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akitoa maelekezo kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Sumbawanga Denis Emanuel (wa kwanza kushoto) juzi . Chuo cha Ufundi Arusha kimepewa mkataba wa ukamilishaji mradi huo ambapo shilingi Bilioni 2 zimetolewa serikali hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa huo wakati walipotembelea kujionea kuanza tena kwa ujenzi wa Chuo cha VETA Sumbawanga ambacho sasa kitakamilika baada ya serikali kutoa shilingi Bilioni 2.035 juzi kufuatia kusimama kwa ujenzi miaka miwili iliyopita.

Serikali imetoa shilingi Bilioni 2.035 kukamilisha mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa (pichani) kilichopo Sumbawanga kupitia fedha za Mpango wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 unaotekelezwa na Wizara ya Elimu.



Na. OMM Rukwa

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa kwa kutoa shilingi Bilioni 2.035 kazi ambayo imeanza tayari.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki (04.02.2022), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema Rais Samia Suluhu Hassan tayari amekwishatoa fedha hizo ambapo kazi imeanza kupitia Mshauri Mkandarasi Chuo cha Ufundi Arusha.

“Tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi 2,035,364,881 zitakazokamilisha mradi huu wa chuo cha VETA Sumbawanga ambao ulikwama miaka miwili iliyopita. Sasa ndani ya miezi mitatu ijayo mradi unakwenda kukamilika” alisema Mkirikiti.

Mkirikiti alimtaka msimamizi wa mradi huo Chuo cha Ufundi Arusha kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati na kuwa anatakiwa kutoa taarifa ya ujenzi na changamoto atakazopitia kila mwezi ili kutokwamisha jitihada za serikali.

“Hapa tumelaza uchumi mkubwa baada ya mradi kusimamia miaka miwili iliyopita, sasa hatutakubali mradi huu ukwame tena fedha tunazo. Lengo kazi hii ikamilike kwa ubora na kwa wakati ili watu wapate faida ya mradi huu katika kubadilisha hali za kiuchumi za wana Rukwa”, alisisitiza Mkirikiti.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyetembelea eneo hilo la mradi akiwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa, alitaja faida za uwepo wa chuo hicho cha VETA kuwa kitazalisha ujuzi kwa vijana wa Rukwa katika fani za ufundi sanifu, kuchochea ukuaji ajira kwa vijana na akina mama pamoja na ujasiriamali .

Naye Msimamizi wa Kazi za Ujenzi toka Chuo cha Ufundi Arusha Dennis Emanuel alisema wamesaini mkataba wa kazi kuanzia Februari Mosi mwaka huu na kuwa wanatarajia kukabidhi mradi ifikapo mwezi Mei mwaka 2022.

Dennis aliongeza kusema wamejipanga kukamilisha kazi zote kwa kutumia mafundi bora ambapo tayari kazi za kusafisha mazingira na kukusanya vifaa vya ujenzi imeanza.

Mradi wa ujenzi chuo cha VETA Sumbawanga hadi uliposimama ujenzi ulikuwa umejenga mabweni ya wanafunzi, madarasa, vituo vya mafunzo kwa vitendo, mkataba, jengo la utawala na mifumo ya maji na umeme ambavyo vitakamilishwa awamu hii kufuatia serikali kutoa fedha hizo.

Kazi mpya zitakazofanyika sasa ni pamoja na ujenzi wa mabweni mapya miwili pamoja na nyumba ya mkuu wa chuo.

Kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Mpango wa Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TRCP No. 5441).

Mkazi wa Sumbawanga Monica Sokoni anayefanya kazi ya kibarua kwenye mradi huo alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kufanikisha mradi huo kwani imemwezesha tena kupata ajira.
Share To:

Post A Comment: