Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda.
 


Na Godwin Myovela, Singida


ASKOFU wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda amehimiza watawa wote kuelekeza zaidi utume wao kwa kuhangaika na malezi ya watoto, sambamba na kuzungumza na familia zinazowazunguka kama alivyohangaika Bikira Maria na Yosefu kwa mtoto Yesu, ili kwa pamoja na umoja kutengeneza msingi mzuri wa afya ya roho na mwili kwa ustawi wa maadili ya Taifa la Mungu.

Kuhusu mauaji yaliyojitokeza kwenye maeneo tofauti nchini, hivi karibuni, sanjari na wimbi la biashara haramu za usafirishaji binadamu, alisisitiza kuwa matendo hayo ni kiashiria cha kulega-lega kwa jukumu la kila mmoja kwenye malezi na makuzi ya watoto ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hali ambayo hatimaye inazalisha matokeo hasi ya kimaadili ndani ya jamii.

Mhashamu Mapunda aliyasema hayo jana-jimboni hapa- kupitia homilia yake kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya watawa wote waliowekwa wakfu kwa Mungu, ambayo hufanyika kila Februari 2 ya kila mwaka kwa lengo la kuomba na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya utume na utumishi wao.

“Tusijifungie tu ndani twende tukawashirikishe watu karama zetu ili ziwaguse na kuwasaidia, tuwape faraja, upendo, tumaini, mwanga, wokovu, tuzungumze na tuwe karibu na familia zinazotuzunguka kwa msaada wa sala bila kuchoka kama walivyofanya Simeoni na Anna pale hekaluni, ili tuokoe jahazi hili la kuporomoka kwa maadili, mauaji na biashara haramu za usafirishaji binadamu,” alisema.

Aidha, kupitia homilia hiyo aliwatia moyo watawa hao kuongozwa na maisha ya unyenyekevu, upendo, amani, uvumilivu, ushirikiano na kuishi kwa fadhila ya usafi wa moyo kwa kuzingatia wote ni askari wa Kamanda mmoja-ambaye ni Kristu-katika muktadha ule ule wa kumfanya apendwe na ajulikane ulimwenguni.

Mhashamu Mapunda pamoja na mambo mengine, aliwakumbusha watawa hao wote wa kike na kiume kuguswa zaidi na maisha ya upendo sambamba na kutoa ushuhuda wa imani, huku akimtaka kila mmoja kuwa zawadi kwa mwingine, jambo ambalo litachagiza furaha na upendo miongoni mwao katika maisha yote ya utume wao.

Alisema, Utukufu wa Mungu ni binadamu aliye hai hivyo kuna kila sababu ya watawa hao kuendelea kuenzi na kuheshimu utu wa kila binadamu bila ya kubagua wala upendeleo wakati wa kuwahudumia; ikizingatiwa kwamba utume unaobagua watu sio utume wa Mungu, na binadamu wote ni mali ya Mungu na wameumbwa kwa sura na mfano wake.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza watawa hao kuhakikisha ajenda ya utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yote yanayowazunguka inazingatiwa na kupewa msukumo wa kipekee sababu kama mazingira yataharibika basi uhai wa binadamu utapotea.

“Amecea (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na Kati) kwa mwaka huu, ambayo Tanzania ni mwenyeji, moja ya ajenda yake ni mazingira…nawasihi sana watawa tujali, tuyatunze, tuyaenzi na kuheshimu mazingira kama nyumba ya Mungu, na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamtukuza Mungu;, kinyume chake tutakufa,” alisema Mhashamu Askofu Mapunda

Jimbo Katoliki Singida kwa sasa lipo kwenye maadhimisho ya matukio mbalimbali kuelekea kilele cha Jubilei yake ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake (1972-2022), ambapo pamoja na mambo mengine, imeelezwa wakati huo jimbo likianzishwa kulikuwa na mashirika 6 pekee ya kitawa, na sasa idadi yake ni zaidi ya 30.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: