Na Asila Twaha, TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli amewataka wachezaji wa netiboli TAMISEMI QUEENS kuzingatia nidhamu na wacheze kwa kujituma katika kipindi chote cha michuano ya ligi ya netiboli ya Muungano.
Akizungumza na wachezaji hao leo Jijini Dodoma wakati akiwaaga kuelekea Zanzibar kushiriki ligi mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza kesho Januari 29, 2022 Mweli amesema kuwa, nidhamu ndio msingi wa mafanikio katika michezo hivyo amewataka wachezaji hao kuiwakilisha vyema Ofisi ya Rais –TAMISEMI katika nidhamu na ushindi.
“Najua kombe tutachukua sababu sisi ni washindi kila siku ila zingatieni nidhamu na uadilifu katika kipindi chote cha michuano, mkumbuke mnaiwakilisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI, tunataka tusikie TAMISEMI Queens sio kwamba inacheza vizuri tu lakini pia kwa nidhamu inaongoza, nidhamu ni sehemu ya ushindi” amesema Mweli.
Aidha, ameupongeza uongozi wa TAMISEMI Sports Club kwa kujituma na kuwekeza muda wao ili kuhakikisha timu hiyo inapata mahitaji yote muhimu katika ligi zilizopita na kuwataka kuendeleza ari hiyo ili mafanikio hayo yawe endelevu.
“Niwapongeze viongozi mnaosimamia timu hii, mnajitoa sana nimeona katika ligi zilizopita umoja wenu na kujituma kwenu kumeleta matokeo mazuri katika timu yetu, niwaombe muendeleze ari hiyo”
amesema Mweli
Pia amewahakikishia wachezaji wa Tamisemi Queens kuwa uongozi wa Tamisemi unatambua jitihada zao katika michezo na wapo tayari kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo walio jipangia.
Naye Timu Kapteni Dafroza Luhwago ameushukuru uongozi wa Tamisemi kwa kuhakikisha timu hiyo inakuwa bora kwenye malezi ya kinidhamu na uchezaji pia ameahidi watarudi na ushindi.
Post A Comment: