Na Pamela Mollel,Hifadhi ya Nyerere
Tanzania kwa sasa ndio nchi yenye hifadhi kubwa kupita zote Barani Afrika kwa mujibu wa wataalamu wa sekta za uhifadhi.
Hifadhi mpya ya Nyerere yenye eneo la kilometa za mraba 30,893 imethibitishwa rasmi kuwa ndio kubwa Zaidi katika ukanda wa Afrika mashariki na Kati.
Kaimu mhifadhi mkuu, Dokta Emilian Kihwele anaeleza kuwa kijiografia, Nyerere imo ndani ya mikoa mine, ikiwemo ya Pwani, Lindi, Ruvuma na Morogoro.
Nyerere pia inashikilia nafasi ya pili kwa ukubwa Barani Afrika baada ya ile ya Namib Naukluft, ya nchini Namibia yenye eneo la kilometa za mraba 49,000.
Kwa mujibu wa Mshauri wa uhifadhi wa Wanyamapori, Maliasili na Mazingira wa shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS), Dokta Asantaeli Melita, Hifadhi ya Nyerere pia ndio eneo lenye idadi kubwa Zaidi ya Tembo nchini.
“Tulifanya sensa ya kuhesabu wanyamapori katika eneo zima la Nyerere na Selous mwaka 2018 na tukagundua kuwa sehemu hii ina tembo takriban 30,000,” alisema Dokta Melita.
Hapa nchini pia Hifadhi ya Nyerere inaongoza kwa Ukubwa baada ya kuipiku ile ya Ruaha ambayo kwa sasa ni ya pili kwa ukubwa nchini.
Hifadhi ya Ruaha pia ndio ya pili kwa ukubwa katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na eneo la kilometa za mraba 20,226.
Hifadhi zote mbili zinazoongoza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki zinapatika upande wa kusini mwa Tanzania ambako kwa bahati nzuri ndiko Tanzania inakotekeleza mradi maalum wa kuendeleza utalii na uhifadhi endelevu kwenye mzunguko wa kusini, yaani REGROW unaofadhiliwa na benki ya dunia.
Mwaka uliopita Hifadhi ya Nyerere ilizalisha 3.1 billioni za kitanzania. Kwa mujibu wa mhifadhi mkuu, wa Nyerere, hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, hifadhi hiyo itakuwa imezalisha Zaidi ya Bilioni 3.6.
Tanzania ina hifadhi za taifa 22 na kati ya hizo, hifadhi ya Serengeti, iliyo ya tatu kwa ukubwa nchini ndio maarufu Zaidi.
Post A Comment: