Na. Angela Msimbira TANGA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema Ofisi ya Rais –TAMISEMI itasimamia kikamilifu utekelezaji wa afua za Lishe kwenye Sekretarieti za Mikoa na Malaka za Serikali za Mitaa.
Akiongea leo katika Mkutano Mkuu wa saba wa Wadau wa masuala ya lishe nchini uliofanyika Jijini Tanga Waziri Ummy amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaahidi kusimamia utekelezaji wa mpango wa afua za lishe kwa kutenga kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano, lengo ni kupunguza udumavu wa ukuaji wa watoto katika jamii kwa kuimarisha lishe bora nchini.
Waziri Ummy anaendelea kufafanua kuwa fedha hizo zitatengwa katika fungu la maendeleo kwa kuwa katika mkakati wa kuimarisha lishe nchni ofisi ya Rais - TAMISEMI inatakiwa kuchangia asilimia 10.5 sawa na kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 67.2 kwa miaka mitano, hivyo suala hilo litatekelezwa kikamilifu.
Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itasimamia fedha zilizopangwa kwa ajili ya shughuli za lishe kwenye Halmashauri zote 184 nchini na kutoa taarifa za mapato na matumizi ya Halmashauri kwa mwaka ikiwemo asilimia kumi kwa ajili ya mikopo ya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itahakikisha fedha ambazo zimetengwa kwenda kutatua afua za lishei zinatumika kama zilivyoelekezwa na kuhakikisha inazibana Halmashauri ambazo hazijatoa fedha hizo kwa wakati.
Amesema itaendelea kusimamia utendaji wa afua za lishe katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufanya tathmini ya mikataba ya lishe iliosainiwa na Wakuu wa Mikoa kote nchini kuanzia ngazi ya Kitaifa, Mikoa, Vijiji, Kata na vitongoji na kuhakikisha na kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote.
Waziri Ummy amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI itasimamia utoaji wa taarifa zenye ubora na wakati kuhusu afua za lishe kwa wakati kupitia mfumo wa utoaji wa taarifa wa intergreted monitoring and evaluation system unaosimamiwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kipindi cha robo mwaka na taarifa hizo zitatumwa kwenye mfumo wa National multsectrol Management Information system unaosimamiwa na taasisi ya chakula na lishe kwa ajili ya kupata taarifa kitaifa.
Aidha, amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi au maafisa waliochini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa uzembe wa utekelezaji na matumizi mabaya ya fedha za lishe zitakazobainishwa.
Post A Comment: