Joachim Nyambo,Mbeya.
WANAUME jijini Mbeya wamehimizwa kuongeza juhudi za kushirikiana na wake zao kwenda kliniki wakati wa ujauzito ikiwa ni sehemu ya kudumisha upendo ndani ya familia na kuweka msingi wa malezi bora.
Meya wa jiji la Mbeya,Dulmohamed Issa alitoa rai hiyo alipozungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya siku ya wanaume duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Novemba 19 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu yake ni iishi kaulimbiu ya siku ya wanaume duniani mwaka huu inayosema ni ‘Mahusiano mazuri kati ya wanaume na wanawake’.
Issa alisema Mahusiano mazuri baina ya mwanaume na mwanamke yanapaswa kutumiwa kama nguzo ya maisha bora ndani ya familia na ili kuyafanya yawe imara ni muhimu yakaongeza kasi ya upendo wakati wa kuanza kutengeneza family hasa kwenye ujauzito.
Alisema ushiriki wa baba wa familia katika masuala ya afya ya uzazi ikiwemo kumsindikiza mkewe kliniki kunajenga mahusiano bora na yenye kudumisha upendo na amani wakati wa ujauzito,mtoto anapozaliwa na hata kadiri familia itakavyoendelea kuishi na kumlea mtoto wao kwa umoja.
Alisema kama kiongozi hapendelei kuona wanaume wanaendelea kuwaachia wanawake jukumu la masuala ya afya ya uzazi na kusisitiza kuwa ni wakati wa jinsi zote kushiriki ili kuwezesha kuwa na jamii yenye ustawi.
“Nitoe wito kwa wanaume wenzangu kwamba jamani mtoto wakwetu wote…ule mzigo tukimwachia mama peke yake si sahihi..Wakati wa ujauzito ni wakati wa kuwa naye karibu,umwoneshe mapenzi.Na hapo ndipo tutakapokuwa tumeanzisha msingi imara wa kaulimbiu ya siku ya wanaume duniani mwaka huu inayosema Mahusiano mazuri kati ya wanaume na wanawake.”
“Tatizo mwanaume akishapata raha mwanzo basi… halafu mtoto akizaliwa utasikia ni wa mama..ndiyo atakuwa wa mama kwa sababu na wewe mwanaume haukuonesha mapenzi wakati wa ujauzito.Ulipaswa kuonesha mahusiano mazuri mama aridhike.” Alisisitiza.
Akitoa taswira halisi ya jiji la Mbeya juu ya mahusiano ya wanaume kwa wake zao kwenye masuala ya uzazi,Mganga mkuu wa jiji hilo,Dk Jonas Lulandala alisema bado ushiriki uko chini na ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau kulishughulikia.
“Tatizo lipo lakini tumejaribu namna ya kuanza kulipunguza ili wanaume waweze kushiriki kwenye masuala ya huduma za uzazi.Kuna umuhimu wake kama baba atashiriki kwenye masuala ya elimu ya uzazi lakini pia akajua huduma ya uzazi inatolewaje.”
“Baba kama atashiriki kwenye suala zima la huduma ya uzazi..akifika pale kliniki atapata elimu..atajua ni lini waweze kuzaa yeye na mke wake ..wazae watoto wangapi na waweke utofautishi wa mtoto mmoja hadi mwingine kwa muda gani.”
Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Iyunga jijini Mbeya ,Dk Yusta Ndotela na Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya cha Nzovwe,Dk Leticia Mgeta walikili bado mwamko ni mdogo kwa wanaume kujihusisha na masuala ya uzazi kwa wake zao wakati wa ujauzito wengi wakiwa na hofu ya kuchekwa na jamii wakiwasindikiza wake zao kliniki.
Post A Comment: