Mtafiti Mkuu wa mradi wa Maji kwa ajili ya Mazingira EFLOW Profesa. Japhet Kashaigili akifafanua jambo kwa viongozi wa Ushirika wa Igomelo.
Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Igomelo, Yohana Ernest akitoa maelezo kwa watafiti kuhusiana na skimu ya umwagiliaji ha Igomelo.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Maji kwa ajili ya Mazingira EFLOW Profesa Japhet Kashaigili akifanya zoezi la uchaguzi wa maeneo ya kukusanya taarifa za mradi.
Profesa Kashaigili akiwa katika banio la skim ya umwagiliaji ya Igomelo alipotembelea skimu hiyo.
Mtaalamu wa Ubora wa Maji Rajabu Mohamedi (kushoto) akichukua sampuli za maji kwa ajili ya utafiti wa ubora wa maji.

Papilon Mkome (kushoto) akichukua taarifa za mimea iliyotambuliwa katika zoezi la kukusanya taarifa za mimea ya Mto Mbarali. Katikati ni Dkt. Emmanuel Mwakinunu na kulia ni Mtaalamu wa Mimea Yahya Mafumbi.

Utafiti ukiendelea.Mtafiti Nyemo Chilagane (kulia) na Fundi Sanifu Haidrolojia Kalister Elizea (katikati) wakifanya urekebishaji (calibration) wa kifaa cha kupimia wingi na mtiririko wa maji (ADCP River_Surveyor )


Na  Amina Hezron, Mbeya


WANACHAMA wa Ushirika wa Kilimo Cha Umwagiliaji Igomelo wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameiomba serikali kupitia Bazara la Taifa na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC)  kuweka alama za mipaka ili kuondoa utata utakaojitokeza katika kusimamia sheria ya mita 60 kutoka kando ya mto kufanya shughuri za kilimo.

Akizungumza katika kikao na watafiti wa Mradi wa utafiti wa Tathimini ya Maji na Mazingira ya Mto Mbarali  Makamu Mwenyekiti wa Ushirika huo Yohana Ernest alisema kuwa kwasasa wananchi wengi wanashindwa kutekeleza agizo hilo kutokana na kukosa uelewa wa namna mita 60 hizo zilivyo huku wengine wakiona uchungu kupunguza wenyewe mashamba yao hivyo wamewataka watu wa mazingira kufanya hivyo wenyewe kwa vipimo halisi.

" si kwamba wakuvunja sheria hawapo wapo lakini ni vizuri tukiwekewa alama ili wakitokea wanaovunja sheria basi tuweze kuwachukulia hatua kwakuvunja sheria yenye kielelezo tayari", alisema Ernest.

Ameongeza kuwa uwepo wa alama hizo za Mipaka (BICON) umesaidia pia kwenye kuzuia wananchi kuvamia maeneo ambayo Bomba la Mafuta la TAZAMA limepita na katika maeneo ambayo yamepita nguzo za shirika la kusambaza umeme nchini TANESCO hivyo wanaanini kutasaidia kuondoa utata.

“ Unajua unaposema mita 60 kuna kuwa na utata sana maana nani apime hizo mita kwani kuna wengine wana hatua fupi na wengine ndefu na wengi wetu tunatumia vipimo vya miguu kwahiyo itaendelea kuleta utata siku hadi siku lakini BICON zitapunguza Kama sio kumaliza kabisa changamoto hiyo ya kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Kota 60 kutoka ukingo wa mto” alifafanua Ernest.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Ushirika wa Skimu ya umwagiliaji ya Igomela ametaja changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni katika kujua ni miti gani inafaa kupandwa kwenye kingo za mito na ipi haifai maana wamekuwa wakipata elimu tofauti tofauti zinazokinzana akitolea mfano ile ya kuwa matete sio rafiki wa mito na kutakiwa kuichoma moto ili kuindoa.

 Mtafiti Mkuu wa mradi wa Maji kwa ajili ya mazingira EFLOW Profesa. Japhet Kashaigili alisema mradi wao wa utafiti unalenga hasa kuangalia afya ya mto Mbarali Kwa kufanya uchunguzi wa kina wa kisayansi katika ikolojia nzima ya Mto ili kuweza kuja na mapendekezo ya kisayansi ambayo yataisaidia serikali na jamii katika kutunza mto Mbarali.

“ Sisi katika kipindi cha miaka miwili tutakusanya taarifa nyingi mfano Maji, Viumbe hai wanaoishi ndani ya Mto na nje ya mto, Mimea na shughuli zingine za kibinadamu ambazo zinasaidia au kuchangia kwenye kuharibu mtiririko endelevu wa maji ili mapendekezo hayo yaweze kufanyiwa kazi” alibainisha Profesa. Kashaigili.

Profesa Kashaigili pia amewashauri viongozi wa ushirika kukaa na wanachama wao ili kutafuta njia ambazo zitakomesha kabisa shughuli za kibinadamu kandokando ya Mto huo ambazo zinaathiri Kwa kiasi kikubwa afya ya Mto huo ambao una faida kubwa kwao na taifa hasa mchango wake kwenye kutiririsha maji kwenye Mto Ruaha Mkuu pamoja na maji kwenye vituo vya kufua umeme vya Kidatu na Bwawa la Mwl Nyerere.

“Sisi Kama watafiti na Mradi tutaangalia namna ya kushirikiana nanyi katika kuanzisha vitalu vya miti Mizuri ambayo ni rafiki wa mazingira na Mto ili ipandwe kurejesha uoto wa asili kandokando ya Mto na Kwa taarifa isiyo rasmi pengine kutakuwa na muongozo ambao utatoa nafasi ya kupanda Mazao na miti yenye faida Kwa wananchi Kama vile ya matunda ili wakati mnatunza mito pia mnufaike na miti hiyo”aliongeza Profesa Kashaigili.

Akitoa ufafanuzi wa maswala yaliyohusu NEMC  Afisa na Mkaguzi wa Mazingira kutoka Kurugenzi ya Utafiti wa Mazingira Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC,  Elias Chundu amewataka wanachama hao kuanza kuzoea na kutii sheria hiyo ya mazingira ili ufatiliaji wake utakapoanza wasije ona wameonewa kwakuwa ipo kwa nia njema ya kuhakikisha mazingira na maji yanakuwa salama ambayo faida yake ni  kubwa kwa wakazi wa hapo na maeneo mengine ya nchi.

"Si kwamba hakuna shughuri ambazo zinafaa kufanyika katika mita hizo 60 hapana, Mpaka sasa upo mwongozo ambao bado haujatoka rasmi, lakini utakapotoka ni mwongozo ambao umeainisha ni shughuri gani zitakazotakiwa kufanyika ndani ya eneo hilo shughuri ambazo ni rafiki kwa mazingira na haziwezi kuharibu vyanzo vya maji", alisema   Chundu.

Aidha bwana bwana Chundu amewataka kuhakikisha wanafanya shughuri zao kwa ukaribu zaidi na bwana afya wa wilaya ili kuweza kusaidiwa kufamu ni namna gani nzuri itakayowasaidia kuteketeza takataka hatarishi zitokanazo na makopo ya dawa za kilimo ili kuepusha uharibifu wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: