Serikali imesema hakutakuwa tena na biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za kibiashara kama ilivyokuwa hapo awali ili kulinda rasilimali zilizopo kwa kuhakikisha zinaendelea kuchangia katika uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazoenezwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa biashara ya wanyamapori hai imerejea tena nchini Tanzania.
Mhe. Mary Masanja amesema Machi 17, 2016 Serikali ilitoa tamko la kuzuia usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi kutokana na matokeo hasi yaliyokuwa yakiendelea kujitokeza kwenye biashara hiyo ikiwemo ukiukwaji wa Sheria na Kanuni wakati wa ukamataji, utunzaji na usafirishaji wa wanyamapori hai.
Aidha, amesisitiza kuwa wanyamapori hai watakaoruhusiwa kutoka nje ya nchi ni wale tu watakaohusika na shughuli za utafiti wa kisayansi ambapo Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini Tanzania (TAWIRI) ina mamlaka ya kuidhinisha wanyamapori kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi kwa shughuli za utafiti wa kisayansi baada ya kupokea maombi na kuongeza kuwa wanyamapori hao wanaweza kuwa hai au kuchukuliwa sampuli zao ikiwemo damu, kinyesi, mifupa, mkojo au tishu huku akibainisha kwamba.
Mhe. Mary Masanja ameongeza kuwa wanyamapori wengine watakaoruhusiwa kusafirishwa nje watakua ni kwa ajili ya shughuli za Kidiplomasia ambao ni utaratibu wa kawaida kwa mamlaka za nchi kutoa zawadi kwa wakuu au wawakilishi wa wakuu wa nchi rafiki kama sehemu ya kujenga mahusiano ya kidplomasia.
‘’Mamlaka ya nchi huwa inaamua aina na idadi ya wanyama itakayotoa kama zawadi lakini kwa kuzingatia mikataba ya Kimataifa tuliyoridhia kama nchi mfano ni zawadi ya ndege aina ya Tausi iliyotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Kenya na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli’´Amesisitiza Mhe. Mary Masanja.
Aidha, ili kuongeza thamani ya mazao ya wanyamapori na kuepuka dhana ya utoroshwaji wa wanyamapori hai kwenda nje nchi, Serikali imeruhusu kusafirisha nje ya nchi wanyampori waliokaushwa (wasiokuwa na uhai) ambao ni ndege wa aina zote pia Mamalia wadogo kama vile sungura, nguchiro na kicheche.
Katika hatua nyingine Mhe. Mary Masanja amesema Serikali imetoa muda wa miezi mitatu (3) ili kuruhusu wafanyabiashara ambao kwa mujibu wa utaratibu walikuwa tayari na wanyamapori kwenye maeneo yao maalum (mazizi) lakini walisitisha kutokana na zuio la Serikali wakaendelea kuwatuza na kuwahifadhi wanyamapori hao wapate fursa ya kusafirisha pindi Serikali itakapotoa tamko rasmi na kuainisha utaratibu utakaotumika kupitia Tangazo la Serikali.
Amesema wanyamapori hai wanaohusishwa katika usafirishwaji katika kipindi cha mpito ni makundi ya wadudu (invertebrates) na wanyamapori jamii ya ndege, reptilia, mamalia na amphibia, ambao jumla ni aina 617 za wanyamapori walioko kwenye mazizi.
Post A Comment: