NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme akiwa amepanda pikipiki iliyotengenezwa na mjasiriamali mwenye ulemavu, Selestine Mkandara ambaye ni mnufaika wa fedha za mikopo zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Misssenyi.


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Christina Mndeme, akichomelea kitanda cha chuma kilichotengenezwa na mjasiriamali mwenye ulemavu, Selestine Mkandara.

...................................................................................

NA MUSSA YUSUPH,MISSENYI

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christine Mndeme, amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ndiyo pekee yenye kutoa mikopo kwa wajasiriamali pasipo kutoza riba tofauti na serikali zingine duniani.

Kwa sababu hiyo amewataka vijana, wakinamama na wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo kwa sababu fedha zipo na zinatolewa kwa waliokidhi vigezo.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani hapa wakati akizungumza na wajasiriamali wanufaika wa fedha za mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na Halmashauri ya Missenyi, Mkoa wa Kagera.

“Tunasema pochi la mama limefunguka, fedha zipo zichangamkieni. Ni serikali gani ambao inatoa mikopo bila riba duniani?. Ni serikali ya Rais Samia pekee ndio inatoa mikopo bila riba kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wake,” alieleza huku akishangiliwa na wanufaika wa mikopo hiyo.

Alizitaka halmashauri kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu ambao wanaujuzi wa kushiriki miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule na afya inayotekelezwa na serikali.

“Ipo miradi ya ujenzi wa madawati, madirisha kwenye shule. Kama kuna wenye ulemavu wana uwezo wa kuitekeleza wapewe na hii itasaidia zaidi kuwainua kiuchumi,” alieleza.

Alisema Ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza itatoa ajira rasmi na zisizokuwa rasmi kwa makundi yote na ndio sababu ya kuanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali kupitia halmashauri.

Mndeme alieleza kuwa wanufaika wa mikopo hiyo ni muhimu wakatumia kwa malengo waliyokusudia pamoja na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Aliziagiza halmashauri kuendelea kutoa mikopo na elimu kwa wajasiriamali kuchangamikia fursa za masoko yaliyopo hususan katika maeneo ya mipakani.

Alisema Wilaya ya Missenyi ina fursa nyingi za kibiashara zinazoweza kufanyika katika eneo la mpaka wa Tanzania na Uganda ikiwemo vijana wa bodaboda kubeba abiria.

Hata hivyo, aliwataka vijana wa bodaboda kuacha kufanya biashara za magendo mipakani na kusafirisha wahamiaji haramu kwani ni kinyume cha sheria za nchi.

Kwa upande wake, mjasiriamali mwenye ulemavu wa viungo, Selestine Mukandara, alitoa salamu za shukrani kwa Rais Samia kwani wenye ulemavu wamekuwa sehemu ya wanufaika kupitia mikopo hiyo.

Mukandara ambaye anajishughulisha na ufundi wa kuchomelea na kutengeneza majiko, alisema amechukua mikopo awamu tatu kupitia halmashauri ya Missenyi iliyomwezesha kupanua wigo wa biashara yake.

“Safari hii nimechukua sh. milioni mbili ambazo natarajia kuongeza mtaji wa shughuli zangu. Nimeweza kutengeneza milango, pikipiki ya wenye ulemavu na majiko. Lakini pia nimeaandaa andiko la kuanzisha kampuni yangu,” alieleza.

Naye, Mwenyekiti wa Kikundi cha Uaminifu Omukitwe kinachojishughulisha na biashara ya bodaboda, Johannes Patrick, alisema kikundi hicho cha vijana kimepatiwa mikopo wa sh. milioni 15.

Alisema fedha hizo zimetumika kununulia pikipiki ambazo kila mwanachama anazitumia kwa shughuli za kubeba abiria.

“Tunaomba umfikishie salama mama yetu Rais Samia, kwamba fedha zipo na tunazipata. Hapa tunakopa kwa thamani ya bei ya pikipiki sokoni na tunarudisha mkopo bila riba.

Alibainisha kuwa: “Mafanikio ni makubwa kwa sababu mkopo huu ni nafuu kwani marejesho yake sawa na sh. 7,000 kwa siku hadi utakapokamilisha tofauti na pikipiki za watu binafsi ambapo tunatakiwa kutoa hesabu kwa mmiliki sh. 10,000 kwa siku kwa kipindi cha miezi 12 hadi 13.”

Hata hivyo, aliiomba serikali kutatua changamoto ya kutozwa sh. 17,000 kwa mwaka na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) wakati bado pikipiki hizo zinahesabika kama mali ya halmashauri kwa sababu bado hawajakamilisha kurejesha mkopo.

Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, imetoa mikopo ya sh. milioni 302 kwa vikundi 36 vya wakina mama, vijana na wenye ulemavu.

Fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa takwa la kisheria linalozitaka halmashauri nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kutoa mikopo kwa makundi hayo ya wajasiriamali.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: